Mwenendo wa Trump mkabala na jamii ya Waislamu wa Marekani wakosolewa
Zaidi ya asilimia 70 ya Waislamu nchini Marekani wamekosoa namna rais wa nchi hiyo anavyoamiliana vibaya na jamii ya Waislamu nchini humo.
Kituo cha Utafiti yaani Pew Research Center ( PEW) kimetangaza kuwa asilimia 74 ya Waislamu nchini Marekani wameutaja mwenendo wa Rais Donald Trump wa nchi hiyo mkabala na jamii ya Waislamu nchini humo kuwa ni wa kiuhasama huku karibu asilimia 65 ya jamii hiyo wakikosoa namna Rais huyo anavyoiongoza nchi hiyo.
Kituo hicho cha utafiti kimesisitiza kuwa mivutano imeongezeka katika uhusiano kati ya Rais Donald Trump na jamii ya Waislamu nchini Marekani kufuatia kupasishwa marufuku ya kuingia nchini humo raia wa nchi sita za Kiislamu. Matokeo ya utafiti uliofanywa na kituo hicho cha PEW yanaonyesha kuwa Waislamu nchini Marekani wanakabiliwa na ubaguzi mkubwa na kwamba Rais wa nchi hiyo amewaikasirisha na kuitia wasiwasi jamii hiyo ya Waislamu huko Marekani huku raia hao wakibainisha kutokuwa na imani na rais huyo. Hii si mara ya kwanza kwa Waislamu nchini Marekani kutokuwa na imani na Rais kutoka chama cha Republican na kubainisha kutoridhishwa naye. Hii ni kwa sababu Waislamu nchini Marekani walikuwa miongoni mwa wakosoaji wa serikali hata wakati wa utawala wa George W. Bush, Rais mstaafu wa nchi hiyo.