Qatar: Saudi Arabia inaitumia Hija kwa malengo ya kisiasa
Wizara ya Waqfu na Masuaia ya Kiislamu ya Qatar imeituhumu Saudi Arabia kuwa inaitumia vibaya ibada ya Hija kwa malengo yake ya kisiasa.
Taarifa ya Wizara ya Waqfu na Masuala ya Kiislamu ya Qatar imetolewa baada ya televisheni ya Saudia kutoa madai yasiyo na msingi dhidi ya Qatar ikidai kuwa, nchi hiyo imefunga ukurasa wa kuandikisha watu kwa ajili ya kwenda kufanya ibada ya Hija nchini Saudia.
Taarifa iliyotolewa na wizara hiyo imesema: Vyombo vya habari vya Saudi Arabia vinaendeleza uadui dhidi ya Qatar kwa kutangaza habari za uongo. Taarifa hiyo pia imeeleza wasiwasi wake kuhusu usalama wa mahujaji wa Nyumba ya Mwenyezi Mungu na kusema maafisa wa Saudi Arabia hawatoi dhamani yoyote ya kulindwa usalama wa mahujaji.
Awali pia Tume ya Haki za Binadamu ya Qatar ilikuwa tayari umemwandikia barua Ripota Maalumu wa Umoja wa Mataifa katika Masuala ya Uhuru wa Kidini ikisema utawala wa Saudi Arabia unatumia ibada ya Hija kwa malengo ya kisiasa. Qatar imesema katika barua hiyo kwamba, watawala wa Riyadh wanakiuka sheria za kimataifa kutokana na jinsi wanavyosimamia ibada ya Hija na kuitumia vibaya ibada hiyo kwa malengo ya kisiasa.
Baada ya kutokea mgogoro katika uhusiano wa nchi hizo mbili, Saudi Arabia ilitishia kwamba utawazuia raia wa Qatar kwenda Makka na Madina kwa ajili ya kutekeleza ibada ya Hija ambayo ni faradhi kwa kila Muislamu mwenye kuweza.
Saudi Arabia pia mwaka jana iliwazuia raia wa Iran, Syria na Yemen kushiriki katika ibada ya Hija.