Medvedev: Vikwazo vya Marekani dhidi ya Russia ni tangazo la vita
https://parstoday.ir/sw/news/world-i32666-medvedev_vikwazo_vya_marekani_dhidi_ya_russia_ni_tangazo_la_vita
Waziri Mkuu wa Russia amesema kuwa, vikwazo vipya vya Marekani dhidi ya nchi hiyo ni sawa na kutangaza vita vya pande zote dhidi ya nchi yake.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Aug 03, 2017 23:29 UTC
  • Medvedev: Vikwazo vya Marekani dhidi ya Russia ni tangazo la vita

Waziri Mkuu wa Russia amesema kuwa, vikwazo vipya vya Marekani dhidi ya nchi hiyo ni sawa na kutangaza vita vya pande zote dhidi ya nchi yake.

Dmitry Medvedev amesema Russia imejibu mapigo kwa kutayarisha kifurushi cha vikwazo vipya dhidi ya Marekani ambavyo amesisitiza vitaanza kutekelezwa hivi karibuni.

Rais Donald Trump wa Marekani amesaini kuwa sheria ya mpango wa vikwazo uliopitishwa na Bunge la Wawakilishi na Seneti ya nchi hiyo dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Russia na Korea Kaskazini.

Mpango wa vikwazo dhidi ya nchi hizo tatu ulipitishwa wiki mbili zilizopita na Baraza la Wawakilishi na kisha Seneti ya Marekani.

Trump vs Putin

Hata hivyo Trump ambaye amesaini sheria hiyo katika hali ya faragha, mbali kabisa na kamera za wapiga picha, ameeleza wasiwasi wake kuhusu athari hasi zinazoweza kutokea kutokana na sheria hiyo ikiwemo kupungua mamlaka ya rais ya kuondoa vikwazo dhidi ya Russia na vilevile kupungua uwezekano wa kupata ushirikiano wa waitifaki wa Washington katika kadhia hiyo.

Marekani imeiwekea Russia vikwazo hivyo kwa kisingizio kwamba Moscow iliingilia uchaguzi wa rais wa mwaka jana nchini Marekani.