Russia: Ugaidi ni hatari kwa dunia nzima
https://parstoday.ir/sw/news/world-i33606-russia_ugaidi_ni_hatari_kwa_dunia_nzima
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Russia amesema kuwa, hatari ya ugaidi nchini Syria ni tishio kwa ulimwengu mzima na kuongeza kwamba, hali ya sasa haihusiani na nchi hiyo ya Kiarabu pekee, bali inajumuisha dunia nzima.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 25, 2017 09:14 UTC
  • Russia: Ugaidi ni hatari kwa dunia nzima

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Russia amesema kuwa, hatari ya ugaidi nchini Syria ni tishio kwa ulimwengu mzima na kuongeza kwamba, hali ya sasa haihusiani na nchi hiyo ya Kiarabu pekee, bali inajumuisha dunia nzima.

Sergey Lavrov amebainisha kwamba, tishio la makundi ya kigaidi ni la kweli na magaidi hao wameonyesha uwepo wao barani Ulaya, Marekani, kusini mashariki mwa Asia na katikati mwa bara hili.

Lavrov amesema kuwa, kile kinachofahamika na kueleweka katika matamshi ya viongozi wa Marekani kinaonyesha kuwa, Washington pia ina utendaji unaofanana na wa Moscow katika kadhia ya Syria na Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Marekani hivi karibuni ilibainisha msimamo kama huo kuhusiana na vita dhidi ya ugaidi.

Marais wa Russia  na Marekani Vladmir Putin (kushoto) Donald Trump

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Russia amezungumzia pia uhusiano wa nchi yake na Marekani na taathira ya uhusiano huo katika kadhia ya Syria na kusema kuwa, Moscow inaamiliana na Washington katika kadhia ya Syria kwa kutazama mambo kwa uhakika wake.

Lavrov ameashiria uhusiano wa nchi yake na Marekani na kusema kuwa, Russia siyo iliyoaanzisha mapambano yasiyo na maana na Washington katika uga wa kimataifa na mlolongo wa uwekaji vikwazo; na inataraji kuona viongozi wa Washington wanaacha munkari na kuwa watu wa kutumia mantiki na akili zaidi.

Ikumbukwe kuwa, uhusiano wa Marekani na Russia umeharibika katika miaka ya hivi karibuni kufuatia mgogoro wa Ukraine na kadhalika madai ya viongozi wa Washington kwamba Moscow iliingilia uchaguzi wa Marekani.