Iran na Russia zajadili usalama wa Bahari ya Caspian
Maafisa wa ngazi za juu wa vikosi vya baharini vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Russia wamekutana na kufanya mazungumzo kuhusu njia za kuimarisha zaidi usalama katika Bahari ya Caspian.
Kamanda Mkuu wa Kikosi cha Majini cha Iran, Admeli Habibollah Sayyari, ameongoza ujumbe wa ngazi za juu wa maafisa wa Jamhuri ya Kiislamu katika mazungumzo na wenzao wa Russia na pande mbili hizo zimeafikiana kuwa, ushirikiano wa nchi zinazopakana na bahari hiyo ni nyeti katika kuimarisha usalama wa maji ya bahari hiyo.
Maafisa hao walikutana na kufanya mazungumzo hayo jana Jumamosi katika mji wa Bali nchini Indonesia, wakati wa duru ya tatu ya mkutano wa kimataifa wa usalama wa baharini (IMSS).
Admeli Sayyari ameongeza kuwa: "Tunaamini kuwa, Bahari ya Caspian, ni bahari ya amani na urafiki; na ili kuimarisha usalama katika maji ya bahari hiyo, hatuhitaji uingiliaji wa nchi za kigeni."
Mbali na kukutana na kufanya mazungumzo na maafisa wa kikosi cha majini cha Russia, maafisa wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wamefanya mazungumzo pia na wenzao kutoka Indonesia, Bangladesh, China, India, Pakistan na Thailand.
Itakumbukwa kuwa, Oktoba mwaka 2015, manowari za Russia zikiwa katika Bahari ya Caspian, zilifyatua makombora 26 ya masafa marefu kupitia anga ya Iran yaliyolenga ngome za Daesh ndani ya ardhi ya Syria.