Aug 29, 2017 07:42 UTC
  • 14 wauawa, kujeruhiwa katika shambulizi karibu na ubalozi wa US, Kabul

Habari kutoka Afghanistan zinasema, kwa akali watu watano wameuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa kufuatia shambulizi la bomu lililotokea karibu na ubalozi wa Marekani mjini Kabul hii leo.

Basir Mujahid, msemaji wa Mkuu wa Polisi mjini Kabul amesema, bomu hilo limeripuka nje ya benki mjini Kabul karibu na ubalozi wa Marekani, ambapo watu tisa pia wamejeruhiwa.

Habari zaidi zinasema kuwa, shambulizi hilo limelenga mkusanyiko wa wafanyakazi hususan maafisa usalama, waliokuwa wamekusanyika nje ya benki hiyo kwa ajili ya kupokea mishara yao.

Hadi tunaenda mitamboni, hakuna kundi lolote lilikuwa limekiri kuhusika na hujuma hiyo ya kigaidi, ingawaje mashambulizi ya namna hii yamekuwa yakifanywa mara kwa mara na genge la kigaidi la Taliban.

Majeruhi wakitolewa katika eneo la mripuko Kabul

Mwishoni mwa mwezi uliopita, zaidi ya watu 40 waliuawa na wengine 60 kujeruhiwa katika shambulio jingine la kigaidi lililotokea huko Kabul, mji mkuu wa Afghanistan.

Takwimu za Wizara ya Afya nchini humo zinasema kuwa, karibu watu 1,700 wameuawa katika wimbi la mashambulizi ya kigaidi ndani ya miezi sita ya kwanza ya mwaka huu.

Makundi ya Taleban na Daesh (ISIS) yamekuwa yakihusika na hujuma hizo ambazo weledi wa mambo wanazitaja kuwa, ni njama ya madola ya Magharibi ya kutaka kuendelea kuwepo askari wao nchini humo.

Tags