Mogherini na Amano wachunguza mwenendo wa utekelezaji wa makubaliano ya JCPOA
Bi Federica Mogherini Mkuu wa Siasa za Nje wa Umoja wa Ulaya na Yukia Amano Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) jana alasiri walichunguza mwenendo wa utekelezaji wa makubaliano ya JCPOA.
Mogherini na Amano walifanya mazungumzo hayo pambizoni mwa Mkutano kwa jina la "Bled Strategic Forum" huko Slovenia zikiwa zimepita siku kadhaa baada ya kuchapishwa ripoti mpya ya msimu na wakala huo kuhusu mchakato wa utekelezaji wa makubaliano ya JCPOA.
Wakala wa IAEA Alhamisi iliyopita kwa mara nyingine tena ulithibitisha katika ripoti yake ya nane ya msimu kwamba, Iran imetekeleza ahadi zake zote kuhusu makubaliano hayo ya nyuklia. Kabla ya hapo pia, Umoja wa Mataifa na Baraza la Usalama la Umoja huo zilikiri kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetekeleza ahadi zake zote kuhusu makubaliano hayo.
Makubaliano ya nyuklia yaliyofikiwa kati ya Iran na kundi la 5+1 linaloundwa na Uingereza, Ufaransa, Russia, Uchina, Marekani pamoja na Ujerumani yametekelezwa kuanzia mwezi Januari mwaka jana; hata hivyo serikali ya Marekani imekuwa ikikiuka makubaliano hayo ikiwa moja ya nchi wanachama wa kundi hilo. Naye Rais Donald Trump wa Marekani ameyataja makubaliano hayo kuwa ni ya kuogofya licha ya misimamo iliyoonyeshwa na pande nyingine husika katika makubaliano hayo na ametaka kuvunjwa makubaliano hayo, hata hivyo jamii ya kimataifa inapinga hatua hiyo ya chuki na uhasama ya Rais wa Marekani.