Harakati ya "Septemba 15" yatoa wito wa kufanyika maandamano makubwa Saudia
Harakati ya Septemba 15 inayoendesha harakati za amani za upinzani nchini Saudi Arabia imetoa wito kwa wapinzano wote wa utawala wa kifalme wa nchi hiyo kushiriki kwenye maandamano ya kupigania matakwa ya wananchi.
Kundi moja lililojitangaza kwenye mitandao ya kijamii kwa jina la "Harakati ya Septemba 15" inayojumuisha wanaharakati wa Saudi Arabia na wapinzani wa utawala wa Aal Saud imetoa taarifa yenye vipengele sita kuhusu misingi na malengo yake na kutoa wito kwa watu wa matabaka yote ya jamii ndani ya Saudia kujiunga na harakati hiyo na kushiriki kwa wingi kwenye maandamano yaliyopangwa kufanyika Ijumaa ya kesho.
Harakati ya Septemba 15 imeashiria malalamiko na matakwa ya wananachi wa matabaka yote nchini Saudi Arabia ikiwemo ukosefu wa ajira, umasikini, watu kuwekwa kizuizini pamoja na wale wanaonyimwa haki zao za kimaada na kimaanawi na kutangaza kuwa harakati hiyo pana inawakilisha watetezi wa uhuru na wazalendo wa Saudia wanaoshuhudia kuangamizwa utajiri wa nchi hiyo kupitia vita vya kieneo au kwa njia ya kuzitunukia hidaya nchi nyengine ikiwemo Marekani na Misri.
Wito wa harakati hiyo unatolewa katika hali ambayo wimbi la utiaji nguvuni maulamaa wa Kiislamu na wanaharakati ambao hawakuiunga mkono serikali ya Riyadh katika mgogoro wake na Bahrain lingali linaendelea kushuhudiwa nchini Saudi Arabia.
Tangu tarehe 5 Juni mwaka huu, Saudi Arabia ikishirikiana na waitifaki wake watatu ambao ni Misri, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na Bahrain zimevunja uhusiano wao wa kidiplomasia na Qatar sambamba na kufunga mipaka yao ya ardhini, baharini na angani dhidi ya nchi hiyo ya Kiarabu.../