Nchi 134 zaunga mkono mapatano ya nyuklia ya Iran
https://parstoday.ir/sw/news/world-i34735-nchi_134_zaunga_mkono_mapatano_ya_nyuklia_ya_iran
Nchi za Kundi la 77 (G77) zimetoa taarifa na kutangaza kuunga mkono mapatano ya nyuklia ya Iran yanayojulikana kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezwaji, JCPOA huku zikisisitiza ulazima wa kuondolewa vikwazo vyote dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 23, 2017 04:29 UTC
  • Nchi 134 zaunga mkono mapatano ya nyuklia ya Iran

Nchi za Kundi la 77 (G77) zimetoa taarifa na kutangaza kuunga mkono mapatano ya nyuklia ya Iran yanayojulikana kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezwaji, JCPOA huku zikisisitiza ulazima wa kuondolewa vikwazo vyote dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Hayo yamebainika katika taarifa iliyotolewa na mawaziri wa mambo ya nje wa nchi wanachama wa G77 pembizoni mwa kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York. Katika taarifa yao, mawaziri wa mambo ya nje wa G77 wamesema JCPOA ni mapatano yanayopaswa kuigwa na ni mfano wa utendaji kazi wenye mafanikio wa mfumo wa pande kadhaa wa kimataifa katika utatuzi wa masuala muhimu ya dunia.

Mawaziri hao wa mashauri ya kigeni kutoka nchi 134 katika taarifa yao pia wamesisitiza ulazima wa kuondolewa vikwazo vya kiuchumi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Kikao cha mawaziri wa mashauri ya kigeni wa G77 kimefanyika Ijumaa na kuhudhuriwa na Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na pia Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.  

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni kati ya wanachama wa G77 na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araqchi alihutubu katika kikao hicho kwa niaba ya Iran. G77 ilianziswa mwaka 1964 na nchi 77 zinazostawi na sasa kundi hilo limepanuka na lina wanachama 134.

Wakati huo huo Ghulamali Khoshroo, Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa amesema baada ya hotuba dhidi ya Iran na iliyojaa utata ya Rais Trump wa Marekani katika Baraza Kuu la umoja huo siku ya Jumanne kwamba nchi za G77 zimetangaza kuunga mkono kikamilifu mapatano ya nyuklia ya Iran na kutaka nchi hii iondolewe vikwazo.