Safari ya ujumbe wa Korea Kaskazini nchini Russia
Katika kushadidi mgogoro kati ya Marekani na Korea Kaskazini, ujumbe wa ngazi za juu wa Pyongyang umefanya safari nchini Russia kwa ajili ya kufanya mazungumzo na viongozi wa taifa hilo.
Choe Son Hui, Mkuu wa Kitengo cha Masuala ya Amerika ya Kaskazini ambacho kiko chini ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Korea Kaskazini ndiye anaongoza ujumbe huo nchini Russia. Safari hiyo imefanyika katika hali ambayo vita vya maneno kati ya Rais Donald Trump wa Marekani na Kim Jong-un, Kiongozi wa Korea Kaskazini, vimezidi kupamba moto, huku serikali ya Pyongyang ikiyataja maneno ya hivi karibuni ya Trump ya kutaka kuisambaratisha Korea Kaskazini kuwa ni tangazo la vita dhidi yake. Katika mazingira hayo, safari ya ujumbe wa ngazi za juu wa Pyongyang mjini Moscow ni umuhimu na ya kuzingatiwa.
Hii ni kwa kuwa, Russia kwa kushirikiana na China zinahesabiwa kuwa washirika wakubwa wa Korea Kaskazini dhidi ya Marekani. Pamoja na hayo ni kwamba, Moscow baada ya kusambaratika Shirikisho la Urusi ya zamani, ilivunja mikataba ya kijeshi na uungaji mkono wake wa upande mmoja kwa Pyongyang, huku ikielekea zaidi upande wa Magharibi. Hata hivyo katika miezi ya hivi karibuni, uungaji mkono wa viongozi wa Russia kwa Korea Kaskazini dhidi ya vitisho vya Marekani, kwa mara nyingine umeifanya Pyongyang kupata matumaini ya ushirika wa Moscow kwa maslahi yake. Hivi karibuni viongozi wa Kremlin katika radiamali yao juu ya vitisho vya Marekani dhidi ya Korea Kaskazini walitangaza kuwa, nchi hiyo ya Asia imefikia kiwango cha juu cha uwezo wa kijeshi kiasi cha kuifanya Marekani isiweze kuishambulia kijeshi.
Pamoja na kwamba msimamo huo wa Russia unaweza kuipa moyo Korea Kaskazini kutokana na vitisho vya Marekani, lakini Pyongyang inataka kupata taarifa zaidi za uungaji mkono wa Moscow kwake hasa ikiwa mashambulizi hayo ya Washington yatatekelezwa dhidi yake. Suala hilo linapata umuhimu zaidi ikitiliwa maanani kwamba, Rais Donald Trump wa Marekani, ni mtu asiyetabirika na ambaye anaweza kutekeleza kitendo hicho cha kijuba cha kuanzisha mashambulizi dhidi ya Korea Kaskazini. Jimy Tarabay, mtaalamu wa masuala ya kisiasa ya Asia ambaye ni raia wa Marekani anasema: "Licha ya kuwa huenda Kremlin isiwe mtetezi bora na muhimu wa Pyongyang katika vita vipya, lakini kudhihiri kwake katika eneo ni aina nyingine ya juhudi za Rais Vladmir Putin wa Russia za kuingia katika mlingano wa jografia ya kisiasa, dhidi ya Marekani." Mwisho wa kunukuu.
Kwa vyovyote vile, hata kama uwezo wake katika sekta ya nyuklia na makombora ya balestiki haijaonyesha kuzitegemea Russia na China, lakini inaonekana kuwa Korea Kaskazini kabla ya kuingia vitani na Marekani kwanza inataka kufanya mazungumzo na washirika wake kwa ajili ya kutumia njia za kisiasa badala ya za kijeshi katika kutatua mgogoro uliopo baina yake na Marekani. Katika uwanja huo inadhaniwa kuwa, China na Russia ambazo ni mihimili miwili muhimumu katika Baraza la Uslama la Umoja wa Mataifa, zitaweza kuchukua hatua chanya kwa manufaa ya Pyongyang. Kuhusiana na suala hilo, Andrei Beclitsky mtaalamu wa masuala ya kisiasa wa nchini Russia anasema: "Miamala hiyo mipya inaweza kupelekea kufikiwa makubaliano ya pande mbili ambapo Korea Kaskazini itasitisha majaribio yake ya makombora mkabala na kuondolewa taratibu vikwazo dhidi yake.
Kama ambavyo pia itatakiwa kukabidhi miradi ya silaha zake za nyuklia kwa usimamizi wa kimataifa." Mwisho wa kunukuu. Kwa vyovyo vile, safari ya ujumbe wa ngazi za juu wa Korea Kaskazini nchini Russia, imefanyika kwa malengo ya utatuzi wa kisiasa wa mgogoro wa nyuklia katika Peninsula ya Korea sambamba na kupunguzwa mashinikizo ya kisiasa na kijeshi ya Marekani dhidi yake. Siasa ambazo zinaungwa mkono na duru za kisiasa na vyombo vya habari ambapo zinaweza pia kumshinikiza Trump ahitimishe vita vya maneno dhidi ya Korea Kaskazini.