Safari ya Rais wa Marekani nchini Cuba
(last modified Mon, 21 Mar 2016 16:18:45 GMT )
Mar 21, 2016 16:18 UTC
  • Rais Obama ziarani Cuba
    Rais Obama ziarani Cuba

Rais Barack Obama wa Marekani Jumapili ya jana aliwasili Havana mji mkuu wa Cuba katika safari ya kihistoria.

Katika safari hiyo Obama anakutana na kufanya mazungumzo na mwenyeji wake Raul Castro na wadau wa sekta binafsi. Hii ni safari ya kwanza kufanywa na Rais aliyeko madarakani wa Marekani nchini Cuba baada ya kupita miaka 88.

Katika mazungumzo yake na wafanyakazi wa ubalozi uliofunguliwa tena hivi karibu wa Marekani mjini Havana, Obama amesema kuwa hiyo ni "fursa ya kihistoria" ya kuweka kando uhasama wa kipindi cha Vita Baridi baina ya nchi hizo mbili.

Chini ya upatanishi wa Vatican na baada ya mazungumzo ya siri ya miezi 18, tarehe 17 Disemba mwaka 2014 Marekani na Cuba zilitoa taarifa ya pamoja zikitangaza kuwa zitaanzisha tena uhusiano wa kidiplomasia. Vilevile ziliwaachia huru wafungwa wa pande mbili. Baada ya hapo, Aprili mwaka 2015 Rais Barack Obama wa Marekani alifanya mazungumzo rasmi na mwenzake wa Cuba, Raul Casrto na huo ulikuwa mkutano wa kwanza wa viongozi wa nchi hizo mbili tangu mwaka 1956. Pande hizo mbili zimefanya mazungumzo kadhaa tangu baada ya tangazo la kuanzishwa uhusiano rasmi lililotolewa Disemba 17 mwaka jana na kwa utaratibu huo kumeandaliwa mazingira kukomesha miaka 55 ya uhasama na uadui wa nchi mbili na kuanzisha tena uhusiano wa kidimplomasia. Hata hivyo ushahidi unaonesha kuwa, Washington haijabadili mienendo yake ya kiadui kuhusiana na Havana na imekuwa ikifanya jitihada za kuingia mambo ya ndani ya Cuba.

Uhusiano wa Marekani na Cuba ulivurugika baada ya ushindi wa mapinduzi ya Cuba mwaka 1959 na kushika hatamu za uongozi Fidel Casrto na hatimaye ulikatwa kabisa mwaka 1961. Baada ya mapinduzi ya Cuba chini ya uongozi wa Fidel Castro, Marekani ilianza kutekeleza siasa za kihasama na kiadui dhidi ya nchi hiyo na baada ya kufeli jaribio la mapinduzi dhidi ya serikali ya ya Castro katika tukio la Ghuba ya Nguruwe (Bay of Pigs), Washington ilizidisha vikwazo vya kiuchumi dhidi ya nchi hiyo. Mwaka 1960 Washinton ilianza kutekeleza vikwazo vya kibiashara, kiuchumi na kifedha maarufu kwa jila la el Bloqueo na vikwao hivyo vinaendelea hadi hivi sasa.

Vikwazo hivyo vya Marekani dhidi ya Cuba vilizuia mjadala mkubwa katika uga wa kimataifa na hadi sasa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limetoa maazimio kadhaa likitaka kukomeshwa vikwazo hivyo vya kidhalimu.

Inaonekana kuwa licha ya madai ya Rais Barack Obama katika uwanja wa kutazama upya mwenendo wa Marekani kuhusu Cuba, Washington itadumisha siasa zake za kijadi mkabala wa Havana yaani vikwazo dhidi ya Cuba, siasa ambazo hata Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Marekani, Ben Rhodes, anakiri kwamba zimeshindwa na kugonga mwamba. Tarehe 11 Septemba mwaka 2015 pia Obama aliafiki kurefushwa vikwazo dhidi ya Cuba kwa mujibu wa sheria inayojulikana kwa jina la Biashara na Adui (Trading with the Enemy Act), au TWEA kwa kifupi. Sheria hiyo iliyopasishwa mwaka 1917 na ingali inatumika hadi hii leo, inapiga marufuku kufanya biashara na nchi zinazotambuliwa kuwa ni adui wa Marekani. Kwa hatua yake ya kupasisha sheria hiyo, kwa hakika Obama amesisitiza suala la kudumishwa uhasama wa Washington dhidi ya Cuba na kupuuza mwenendo wa kuanzishwa upya uhusiano baina ya pande hizo mbili katika miezi ya hivi karibuni.

Japokuwa baadhi ya wachambuzi wa mambo walikuwa wakidhani kwamba, mwenendo wa kurejeshwa uhusiano wa kawaida baina ya Marekani na Cuba utashika kasi zaidi baada ya tangazo la kurejeshwa uhusiano na kufunguliwa balozi za nchi hizo mbili, lakini hadi sasa kuna vikwazo ni vizuizi vikubwa katika njia hiyo. Miongoni mwa vikwazo hivyo ni kwamba uhusiano huo una wapinzani wakubwa ndani ya Congresi ya Marekani. Vilevile Wacuba wanaoishi nchini Marekani na lobi yao yenye nguvu kubwa katika Congresi ya nchi hiyo daima wamekuwa wakipinga uhusiano huo.

Alaa kulli hal, safari ya Obama nchini Cuba inatambuliwa kuwa ni hatua muhimu katika uhusiano wa nchi hizo mbili lakini tunaweza kutazamia kuwa, uingiliaji wa Marekani katika masuala ya ndani ya Cuba hususan mjadala kuhusu haki za binadamu na masuala mengine ya kisiasa, kijamii na kiuchumi utaendelea kushuhudiwa, suala ambalo bila shaka litakabiliwa na jibu kali la viongozi wa Havana. Hii ni pamoja na kuwa, Marekani imekataa kuirejeshea Cuba Ghuba ya Guantanamo na suala hilo linaweza kuendeleza hitilafu kati ya pande hizo mbili.