Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa asisitiza umuhimu wa JCPOA
Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amejibu matamshi yaliyotolewa na Rais Donald Trump wa Marekani dhidi ya Iran na makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na kutilia mkazo umuhimu wa kulindwa makubaliano hayo.
Taarifa iliyotolewa na Stephane Dujarric imesisitiza tena msimamo wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres wa kuunga mkono makubaliano ya nyuklia ya Iran na nchi sita wanachama katika kundi la 5+1.
Taarifa hiyo imesema: Katibu Mkuu wa UN amesisitiza mara kwa mara kwamba, makubalioano ya JCPOA ni hatua kubwa katika njia ya kulinda amani na usalama wa dunia.
Wakati huo huo Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Sigmar Gabriel naye amepinga matamshi ya Trump akisema kuwa nchi za Umoja wa Ulaya zinaunga mkono makubaliano ya nyuklia na Iran na kwamba wiki zijazo umoja huo utafanya jitihada za kuishawishi Kongeresi ya Marekani kuhusu udharura wa kulindwa makubaliano hayo.
Vilevile Waziri Mkuu wa Italia, Paolo Gentiloni amepinga matamshi ya Donald Trump dhidi ya Iran na kusisitiza kuwa, kulindwa kwa makubaliano ya JCPOA kunadhamini maslahi ya pamoja ya kitaifa.
Kiongozi wa waliowachache katika Kongresi ya Marekani, Nansi Pelosy pia amepinga matamshi ya Trump dhidi ya Iran na vitisho vyake vya kutaka kujiondoa katika makubaliano ya nyuklia na kusema uamuzi kama huo utakuwa makosa makubwa ambayo yatahatarisha usalama wa Marekani.
Waziri wa zamani wa mambo ya nje wa Marekani, John Kerry pia ameutaja uamuzi wa Rais wa nchi hiyo Donald Trump wa kukataa kupasisha kwamba Iran imeheshimu makubaliano ya JCPOA kuwa ni hatari na ameihimiza Kongresi kulinda makubaliano hayo.
Jana Ijumaa Ikulu ya Rais wa Marekani White House ilitangaza kile kilichoitwa stratijia kamili na mpya ya Rais wa nchi hiyo kuhusu Iran na makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na masaa kadhaa baadaye Donald Trump alitoa hotuba iliyokuwa na maneno ya kukinzana na kudhihirisha tena kinyongo na uhasama wake dhidi ya taifa la Iran.