Marekani yazidi kufanya hali ya mambo Korea kuwa mbaya
(last modified Tue, 24 Oct 2017 14:57:45 GMT )
Oct 24, 2017 14:57 UTC
  • Marekani yazidi kufanya hali ya mambo Korea kuwa mbaya

Marekani imeendelea kufanya hali ya mambo katika eneo la Peninsula ya Korea kuwa mbaya na hivyo kuhatarisha usalama wa eneo hilo.

Hatua hiyo imekuja kufuatia nchi hiyo kuendesha maneva ya kijesha karibu kila siku kwa kisingizio cha kupambana na vitisho vya Korea Kaskazini. Katika uwanja huo, kwa mara nyingine Marekani, Korea Kusini na Japan zimeanzisha maneva mapya ya kijeshi ya siku mbili kwa kisingizio hicho hicho. Shirika la Habari la Korea Kusini (Yonhap) limetangaza kuwa, nchi hizo zimeanzisha maneva mapya Jumanne ya leo kwa lengo la kile kilichotajwa kuwa ni kukabiliana na vitisho vya makombora ya Korea Kaskazini.

Ramani ya eneo la Peninsula ya Korea ambalo sasa linashuhudia hali tata

Hayo ni maneva ya tano ya pamoja kati ya nchi tatu hizo kufanyika katika eneo hilo kuanzia mwezi Juni mwaka huu. Maneva hayo ya siku mbili yameanza katika hali ambayo kwa mara kadhaa Korea Kaskazini imekuwa ikisisitiza kuwa, itaendelea kujiimarisha kwa silaha za nyuklia na makombora ya balestiki madamu chokochoko za Marekani na washirika wake zitaendelea katika eneo hilo. Katika hatua nyingine, Wizara ya Mambo ya Nje ya China imetetea ongezeko la mabadilishano ya kibiashara kati yake na Korea Kaskazini, licha ya vikwazo ambavyo nchi hiyo imewekewa.

Bendera za China na Korea kaskazini kama ishara ya kuendeleza mahusiano yao

Taarifa iliyotolewa na Beijing mapema leo sambamba na kutoa radiamali kwa ukosoaji wa Marekani dhidi yake, imetangaza kuwa itaongeza kiwango cha mauziano ya kibiashara kati yake na Pyongyang. Pamoja na hayo imesisitiza kuheshimu vikwazo vya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa dhidi ya Korea Kaskazini. China imeongeza kuwa, itaendelea kuheshimu tu vikwazo vinavyohusu silaha za Korea Kaskazini na si vinginevyo.

Tags