Mwaka 2017 watarajiwa kuvunja rekodi ya kuwa na joto kali
https://parstoday.ir/sw/news/world-i36196-mwaka_2017_watarajiwa_kuvunja_rekodi_ya_kuwa_na_joto_kali
Mwaka huu 2017 unatarajiwa kawa miongoni mwa miaka mitatu iliyovunja rekodi ya kuwa na jioto kali katika historia ya sayari ya dunia.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Nov 06, 2017 08:00 UTC
  • Mwaka 2017 watarajiwa kuvunja rekodi ya kuwa na joto kali

Mwaka huu 2017 unatarajiwa kawa miongoni mwa miaka mitatu iliyovunja rekodi ya kuwa na jioto kali katika historia ya sayari ya dunia.

Hayo ni kwa mujibu wa ripoti mpya ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Utabiri wa Hali ya Hewa Duniani (WMO) iliyotolewa leo huku dunia ikiendelea kukumbwa na majanga makubwa kama vimbunga, mafuriko, mawimbi joto na ukame kutokana na mabadiliko ya tabianchi.

Ripoti hiyo ya hali ya hewa 2017 inayoainisha athari zake kwa usalama wa binadamu, maisha na mazingira, inasema kuna dalili za muda mrefu za mabadiliko ya tabianchi kama vile ongezeko la kiwango cha hewa ukaa (carbon dioxide), kupanda kwa kina cha maji baharini na ongezeko la kiwango cha tindikali baharini.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa WMO, Petteri Taalas miaka mitatu iliyopita imevunja rekodi ya joto kali duniani, na mwaka huu wa 2017 joto limekuwa wastani wa nyuzi joto 1.1C juu zaidi ya ilivyokuwa kabla ya karne maendeleo ya viwanda.

Bara la Asia linaongoza kwa kufikia nyuzi joto 50C, huku eneo la Caribbean likikumbwa na vimbunga vya kupindukia, mvua za Monsoon nazo zikisababisha mafuriko makubwa Asia, moto wa msituni ukiteketeza maisha na mali Marekani huku katika kanda ya Afrika Mashariki Kenya ikitangaza ukame kama janga la kitaifa 2017.

Ongezeko la joto limesababisha ukame katika nchi nyingi za Afrika

Ripoti hii imetolewa mjini Bonn, Ujerumani  ambapo Katibu Mkuu mtendaji wa mkutano wa Umoja wa Mataifa wa mabadiliko ya tabia nchi UNFCCC Patricia Espinosa amesema takwimu hizi zinaainisha ongezeko la hatari kwa binadamu, uchumi na maisha kwa ujumla. Amesema  endapo dunia itashindwa kutekeleza malengo na maazimio ya makataba wa Paris wa mabadiliko ya tabia nchi basi dunia itakumbwa na maafa makubwa.

Katika hali ambayo Marekani ni kati ya nchi zinazongoza katika uchafuzi wa mazingira na hivyo kusababisha ongezeko la joto juniani kutokana na viwanda vyake, lakini hivi karibuni Rais Donald Trump wa nchi hiyo alikaidia waliowengi duniani na akatangaza kujiondoa katika mkataba wa Paris unaolenga kulinda mazingira.