Mogherini asisitiza tena EU inafungamana na mapatano ya nyuklia ya Iran
https://parstoday.ir/sw/news/world-i37043-mogherini_asisitiza_tena_eu_inafungamana_na_mapatano_ya_nyuklia_ya_iran
Mkuu wa sera za kigeni katika Umoja wa Ulaya kwa mara nyingine amesisitiza kuwa EU itaendelea kufungamana na mapatano ya nyuklia baina ya Iran na kundi la 5+1.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 01, 2017 12:14 UTC
  • Mogherini asisitiza  tena EU inafungamana na mapatano ya nyuklia ya Iran

Mkuu wa sera za kigeni katika Umoja wa Ulaya kwa mara nyingine amesisitiza kuwa EU itaendelea kufungamana na mapatano ya nyuklia baina ya Iran na kundi la 5+1.

Federica Mogherini Mkuu wa Sera za Kigeni katika Umoja wa Ulaya akizungumza leo Ijumaa katika Kongamano la Kimataifa la Mazungumzo ya Mediterania katika mji mkuu wa Italia, Roma, amesema mapatano ya nyuklia ya Iran yajulikanayo kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezwaji JCPOA ni kwa maslahi ya EU na eneo. Ametoa mwito kwa viongozi wa nchi zilizotia saini mapatano ya JCPOA kuyaunga mkono na kuyaimarisha.

Mogherini amesisitiza kuwa, nchi 28 wanachama wa Umoja wa Ulaya zimemfahamisha Rais Donald Trump wa Marekani kuwa utekelezwaji wa JCPOA ni kipaumbele kikuu cha usalama kwa EU.

Aidha amesema mapatano ya nyuklia yana nguvu za azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na hivyo Marekani haiwezi kujiondoa na wala haiwezi kutekeleza baadhi ya vipengee vyake na kuacha vingine.

Pembizoni mwa kikao hicho, Alkhamisi usiku Mogherini alikutana na kufanya mazungumzo na Mohammad Javad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje ya Iran kuhusu masuala mbali mbali ikiwemo kadhia ya nyuklia.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Mohammad Javad Zarif na mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Federica Mogherini

Itakumbukwa kuwa Iran na nchi tano wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa yaani Russia, China, Ufaransa, Uingereza na Marekani pamoja na Ujerumani zilifikia mapatano kuhusu kadhia ya nyuklia ya Iran. Mapatano hayo ambayo ni maarufu kwa jina la JCPOA yalifikiwa Julai 2015 na kuanza kutekelezwa Januari 16 mwaka jana. Kwa mujibu wa mapatano hayo, Iran ilitakiwa kupunguza baadhi ya shughuli zake za nyuklia huku nchi za Magharibi zikitakiwa ziiondolee Iran vikwazo. Lakini pamoja na hayo Marekani inakaidi kutekeleza mapatano hayo huku Rais  Donald Trump wa nchi hiyo akitishia kuiondoa nchi yake katika JCPOA.