Jordan: Uturuki ndio muasisi wa misimamo ya kufurutu mipaka
Mfalme Abdullah wa Pili wa Jordan amesema kuwa Uturuki ndio chimbuko la misimamo ya kufurutu katika eneo la Mashariki ya Kati na bara Ulaya.
Nakala ya siri iliyovuja imefichua kuwa, Mfalme Abdullah wa Jordan aliyasema hayo wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na maafisa wa ngazi za juu wa Marekani Januari 11 mwaka huu.
Gazeti la The Guardian limemnukuu mfalme huyo ambaye alisema kuwa: “Misimamo mikali inazaliwa Uturuki na kwamba nchi hiyo imekuwa ikituma makundi ya watu wenye misimamo ya kufurutu ada kwenda bara Ulaya.”
Mfalme Abudullah II wa Jordan aliwaambia wanachama wa kamati ya Intelijensia na ile Uhusiano wa Kigeni ya Bunge la Seneti ya Marekani kuwa, sio sadfa kwamba kuna idadi kubwa ya magaidi miongoni mwa wakimbizi wanaokimbilia bara Ulaya na kwamba, mpango huo ni katika sera ya Rais Recep Teyyip Erdogan wa Uturuki ya kutuma magaidi barani Ulaya.
Mfalme huyo ameongeza kuwa, mbali na kuunga mkono makundi ya kigaidi nchini Syria, serikali ya Uturuki imeruhusu waasi wenye misimamo ya kufurutu ada kuvuka mpaka wa nchi hiyo na kuingia Syria, nchi hiyo ambayo imeshuhudiwa mapigano kwa takriban miaka mitano sasa, ambapo watu zaidi ya laki 4 na elfu 70 wamekwishauawa.