Kuanza tena safari za ndege kati ya Russia na Misri
Rais wa Russia amesaini dikrii akiamuru kuanza tena safari za kawaida za ndege kati ya nchi hiyo na Misri ambazo zilisimamishwa kufuatia mlipuko uliotokea katika ndege ya Russia katika anga ya mkoa wa Sinai kaskazini mwa Misri.
Hati iliyosainiwa leo na Rais Vladimir Putin wa Russia inaeleza kuwa agizo hilo linajumuisha kutekelezwa hatua maalumu kwa ajili ya kudhamini usalama wa taifa na kuwalinda raia wa Russia mkabala na jinai na vitendo haramu. Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia pia huko nyuma ilitangaza kuwa Misri inapasa kuimarisha hali ya usalama katika viwanja vyake vya ndege ili kuwawezesha watalii kutoka Russia kufanya safari nchini humo.
Tarehe 31 mwezi Oktoba mwaka 2015 ndege ya Russia aina ya Airbus-321 iliyokuwa na abiria 217 na wahudumu saba ilitoweka kwenye rada dakika 23 baada ya kuondoka mjini Sharam Sheikh Misri, saa kumi na moja na dakika 50 ikielekea katika mji wa Saint Petersburg nchini Russia, ambapo watu wote 224 waliokuwemo ndani ya ndege hiyo walipoteza maisha.
Kundi la kigaidi la Daesh lilitangaza kuhusika na ajali hiyo ya ndege. Kufuatia tukio hilo, Russia ilisimamisha safari zake zote za ndege kuelekea Misri.
Idara ya Usalama ya Russia (FSB) wakati huo ilitangaza kuwa, ajali hiyo ya ndege ilitokana na shambulizi la kigaidi.