FAO yataka uwekezaji zaidi katika kupambana na njaa na umasikini
(last modified Fri, 05 Jan 2018 03:51:34 GMT )
Jan 05, 2018 03:51 UTC
  • FAO yataka uwekezaji zaidi katika kupambana na njaa na umasikini

Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) limetoa wito wa kuweko uwekezaji zaidi katika uga wa kupambana na umasikini na njaa ulimwenguni.

Ripoti ya Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) imeyataka mataifa ya dunia kuchukua hatua zaidi za kuwekeza katika uwanja wa kupambana na umasikini na baa la njaa duniani.

Ripoti hiyo iliyotolewa jana Alkhamisi inaonyesha kuwa, kuna watu milioni 815 ulimwenguni wanaotaabika kwa baa la njaa.

Kwa mujibu wa FAO, ongezeko la idadi ya watu wanaotaabika kwa njaa ulimwenguni, kwa kiwango kikubwa chimbuko lake ni kushadidi mizozo, machafuko, vita, vitendo vya utumiaji mabavu na vilevile kubadilika haraka hali ya tabianchi.

Ethiopia ni moja ya nchi za Kiafrika inayokabiliwa na ukame

Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) limeitaka jamii ya kimataifa kutoghafilika na malengo yaliyoainishwa ya kung'oa mizizi ya baa la njaa hadi kufikia mwakak 2020.

Shirika hilo limesisitiza kwamba, ili kufikia malengo hayo kuna ulazima wa kuweko uwekezaji mpya ambao unapaswa kufanywa na serikali na vilevile sekta binafsi.

Takwimu za hivi karibuni kuhusu uzalishaji wa kilimo na bidhaa za chakula za shirika la FAO zinaonyesha kuwa, nchi 37 zikiwemo 29 za Kiafrika zinahitaji msaada mkubwa wa chakula kutokana na kukabiliwa na uhaba wa chakula.

Tags