Katibu Mkuu wa UN aunga mkono makubaliano ya JCPOA
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameunga mkono makubaliano ya nyuklia yanayojulikana kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji JCPOA.
Stephane Dujarric Msemaji wa Antonio Guterres Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa jana aliwabainishia waandishi wa habari taarifa ya Katibu Mkuu wa UN kuhusu makubaliano hayo ya nyuklia. Kwenye taarifa hiyo, Guterres amesema amefurahishwa kuona makubaliano ya JCPOA yakitekelezwa kwa mwaka wa pili na kuongeza kuwa masuala yasiyohusiana na makubaliano hayo ya nyuklia hayapasi kudhuru mapatano hayo ya kimataifa.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesisitiza namna makubaliano ya JCPOA yalivyosaidia amani na usalama wa kieneo na dunia kwa ujumla na kuongeza kuwa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia (IAEA) umethibitisha mara kadhaa kuwa Iran imetekeleza kikamilifu majukumu yake kwa mujibu wa makubaliano hayo.
Wakati huo huo Federica Mogherini Mkuu wa Siasa za Nje wa Umoja wa Ulaya na pia viongozi wa nchi za Ulaya katika miezi ya hivi karibuni walisisitiza mara kadhaa kwamba makubaliano hayo ya nyuklia ni ya jamii ya kimataifa na kuyaunga mkono.
Itakumbukwa kuwa Rais Donald Trump wa Marekani aliyataja makubaliano ya JCPOA kuwa ni ya kutisha kinyume na misimamo iliyodhihirishwa na pande nyingine husika katika makubaliano hayo na amekuwa akitaka kufutwa makubaliano hayo, hata hivyo jamii ya kimataifa inapinga hatua hiyo ya kiuhasama ya Rais wa Marekani.