Katibu Mkuu wa UN atetea makubaliano ya nyuklia ya JCPOA
Katibu Mkuu wa jumuiya kubwa zaidi ya kimataifa ametetea kuendelea kutekelezwa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.
Antonio Guterres amesema katika taarifa iliyotolewa kwa mnasaba wa kutimia mwaka wa pili wa kutekelezwa makubaliano hayo kwamba, maudhui zisizohusiana na makubaliano ya JCPOA hazipasi kutia doa katika mkataba huo wa kimataifa.
Matamshi hayo ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa yametajwa kuwa ni muhimu sana baada ya hotuba ya vitisho iliyotolewa na Rais Donald Trump wa Marekani dhidi ya makubaliano hayo. Siku chache zilizopita Trump alirefusha agizo la kusitishwa vikwazo vya nyuklia dhidi ya Iran lakini aliweka masharti manne ya kubakia Marekani katika mkataba huo. Donald Trump alitishia kuwa, iwapo masharti hayo hayatatekelezwa Marekani itajiondoa katika mkataba wa nyuklia wa JCPOA.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya, Rais wa Ufaransa na Russia zimepinga vikali msimamo huo mpya wa Rais wa Marekani kuhusu mkataba wa nyuklia wa JCPOA. Mkataba huo kwa hakika ni sehemu ya azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kukiukwa kwake kuna maana ya kukiuka azimio la Baraza la Usalama. Hii ni pamoja na kuwa, Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) kama taasisi pekee yenye mamlaka ya kutoa maoni kuhusu miradi ya nyuklia ya nchi wanachama katika Mkataba wa Kuzuia Silaha za Nyuklia (NPT) kwa kifupi, hadi sasa umethibitisha mara 10 kwamba Iran imetekeleza kikamilifu majukumu yake kwa mujibu wa makubaliano ya JCPOA.
Pamoja na hayo yote serikali ya Marekani imeendeleza sera zake za uhasama na ukiukaji wa makubaliano ya kimataifa kwa kutishia kuwa itajiondoa katika makubaliano hayo katika siku 120 zijazo iwapo masharti yake hayatatekelezwa. Itakumbukwa kuwa makubaliano hayo ya kimataifa ni matokeo ya mazungumzo ya miaka miwili ya Iran na kundi la 5+1 linalojumuisha nchi za Uingereza, Ufaransa, Ujerumani, Russia, China na Marekani yenyewe.
Inaonekana kuwa serikali ya Trump inatumia njia ya vitisho ili kuilazimisha Kongresi ya Marekani na nchi zilizoshiriki mazungumzo ya nyuklia kuingiza suala la makombora ya Iran katika mkataba wa nyuklia wa JCPOA. Hata hivyo Iran, Russia, China, Umoja wa Ulaya na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wamesisitiza kwamba, hayo ni masuala mawili tofauti na kwamba makubaliano ya nyuklia ya JCPOA yanapaswa kuendelea kutekelezwa bila ziada wala nakisi.