Warohingya walioko Bangladesh wakataa kurejeshwa nchini Myanmar
Mamia ya wakimbizi wa Kirohingya walioko nchini Bangladesh leo Ijumaa wamefanya maandamano wakipinga mpango wa kuwarejesha nchini Myanmar, ambako walikimbia mauaji na mashambulizi kutoka kwa jeshi la nchi hiyo likishirikiana na Mabudha wenye misimamo mikali.
Licha ya kuishi maisha ya kudhalilisha na hatari katika kambi za wakimbizi zilizoko kusini mashariki mwa Bangladesh, lakini wakimbizi hao wamesema kuwa hawako tayari kurejea nchini kwao.
Wakimbizi hao Waislamu wa Rohingya wamesema watarejea katika mkoa wao wa Rakhine nchini Myanmar kwa masharti mawili; mosi, wadhaminiwe usalama wao na pili wapewe uraia.
Mmoja wa wakimbizi hao amenukuliwa na shirika la habari la AFP akisema kuwa, wapo tayari kurejea nchini Myanmar iwapo kutatumwa kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa hususan katika mkoa wa Rakhine.
Amesema kama tunavyomnukuu, "Tunachotaka ni askari wa kulinda amani wa UN, kupewa uraia na kutekelezewa haki zetu za msingi kama raia wengine wa Myanmar."
Serikali za Bangladesh na Myanmar zilikubaliana hivi karibuni kuanza mchakato wa kuwarejesha wakimbizi hao wa Kirohingya huko Burma, katika kipindi cha miaka miwili.
Mpango huo ambao unatazamiwa kuzinduliwa rasmi Jumanne ijayo, umetajwa na shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International kuwa wa kuharakishwa na wa mapema, ikizingatiwa kuwa, kumbukumbu za mauaji, ubakaji na mateso zingali mbichi katika akili za wakimbizi hao.