Abbas autaka Umoja wa Ulaya kutambua rasmi nchi huru ya Palestina
Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina ameutaka Umoja wa Ulaya (EU) kuharakisha suala la kuitambua rasmi nchi huru ya Palestina.
Mahmoud Abbas alisema katika mazungumzo yake ya jana na Mkuu wa Siasa za Kigeni wa Umoja wa Ulaya, Fededica Mogherini mjini Brassels kwamba kuitambua rasmi nchi huru ya Palestina hakuwezi kukwamisha mazungumzo ya amani ya Mashariki ya Kati.
Amesema kuwa hatua ya Umoja wa Ulaya ya kutambua rasmi nchi huru ya Palestina italihamasisha taifa la Palestina kuwa na matumaini mema na kusubiri amani. Amesisitiza azma ya serikali ya ndani ya Palestina ya kuunda nchi huru moja mji mkuu wake ukiwa Quds tukufu.
Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina pia ameitaka Israel kuheshimu mapatano iliyoyatia saini.
Wakati huo huo nchi nne za Ulaya zinafanya mikakati ya kutambua rasmi nchi huru ya Palestina.
Kanali ya 10 ya televisheni ya Israel uimetangaza kuwa, nchi za Slovenia, Belgium, Luxembourg na Ireland zimeanzisha mikakati ya kuitambua rasmi nchi huru ya Palestina.
Msimamo huo wa nchi mbalimbali dunia kuhusu Palestina unafuatia hatua ya Rais Donald Trump wa Marekani ya kuitangaza Quds (Jerusalem) kuwa ni mji mkuu wa utawala haramu wa Israel kinyume kabisa na maamuzi ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.