Maelfu ya watu waandamana kupinga safari ya Trump nchini Uswisi
https://parstoday.ir/sw/news/world-i39407-maelfu_ya_watu_waandamana_kupinga_safari_ya_trump_nchini_uswisi
Maelfu ya raia wa Uswisi wameandamana mjini Zurich na katika miji mingine muhimu ya nchi hiyo ikiwemo ya Geneva, Lausanne na Fribourg kupinga Rais Donald Trump wa Marekani kuhudhuria kongamano la kila mwaka la Jukwaa la Uchumi Duniani (WEF) linalofanyika katika mji wa Davos.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 24, 2018 04:25 UTC
  • Maelfu ya watu waandamana kupinga safari ya Trump nchini Uswisi

Maelfu ya raia wa Uswisi wameandamana mjini Zurich na katika miji mingine muhimu ya nchi hiyo ikiwemo ya Geneva, Lausanne na Fribourg kupinga Rais Donald Trump wa Marekani kuhudhuria kongamano la kila mwaka la Jukwaa la Uchumi Duniani (WEF) linalofanyika katika mji wa Davos.

Waandamanaji hao ambao wengi wao ni waungaji mkono wa jumuiya za wafanyakazi na wanachama wa chama cha kijani na cha demokrasia ya kisoshalisti nchini Uswisi wamekosoa marufuku ya kuandamana iliyowekwa katika mji wa Davos linakofanyikia kongamano hilo.

Katika siku za hivi karibuni miji mbalimbali ya Uswisi imekuwa uwanja wa maandamano makubwa ya kupinga kuhudhuria Trump kongamano la Jukwaa la Uchumi Duniani.

Mabango yenye ujumbe wa kumpinga Trump

Waandamanaji wamekuwa wakibeba mabango na maberamu yenye jumbe na kualimbiu mbalimbali za kumkosoa na kumpinga rais huyo wa Marekani. Miongoni mwao ni zile zisemazo: "Trump hakaribishwi" na "Mbaguzi Mpenda Ngono Bepari".

Rais huyo wa Marekani anatazamiwa kuhutubia Jukwaa la Uchumi Duniani siku ya Ijumaa. Kongamano hilo lililoanza jana Jumanne linatazamiwa kuendelea hadi Ijumaa ya tarehe 26 Januari.../