Feb 12, 2018 04:35 UTC
  • Matumaini ya kuishi yamepungua nchini Marekani

Imeelezwa kuwa, matumaini ya kuishi nchini Marekani yameendelea kupungua kwa mwaka wa pili mtawalia na kwamba, utafiti unaonyesha kuwa, matumizi ya madawa ya kulevya, unywaji pombe na kuongezeka kiwango cha matukio ya kujiua ni sababu kuu zilizochangia kupungua matumaini ya kuishi miongoni mwa raia wa nchi hiyo ya Kimagharibi.

Ripoti zinaonyesha kuwa utafiti mpya uliofanywa na jarida la masuala ya kitiba la British Medical Journal unaonyesha kuwa, kiwango cha kupungua matumaini ya kuishi ni kikubwa zaidi miongoni mwa Wamarekani weupe na wa jamii za watu wanaoishi vijijini. 

Steven Woolf, mhakiki wa utafiti huo anasema kuwa, takwimu za vifo vinavyotokana na matatizo ya msongo wa mawazo na  na utumiaji mbaya wa dawa pamoja na kujiua zimeongezeka sana nchini Marekani.

Aidha mtaalamu huyo anasema kuwa, kwa mujibu wa uchunguzi huo, Wamarekani wana usalama mdogo mno ikilinganishwa na jamii za nchi nyingine zilizoendelea kutokana na sababu mbalimbali kama maradhi ya ukimwi, unene, utumiaji wa madawa ya kulevya na umiliki wa silaha kiholela.

Aidha ripoti ya utafiti huo inaeleza kwamba, katika mwaka 2016 kiwango cha matumaini ya kuishi nchini Marekani kilikuwa asilimia 78.6 ambacho ni kidogo kwa asilimia 0.10 ikilinganishwa na mwaka wa kabla yake yaani 2015.

Utafiti huo unaeleza pia kwamba, bado hakujatolewa takwimu zinazoonyesha kiwango cha matumaini ya kuishi katika mwaka uliopita wa 2017.

Kadhalika utafiti huo unabainisha kwamba, kutokuweko uangalizi wa masuala ya afya kwa jamii nchini Marekani ni miongoni mwa sababu zinazochangia kupungua kiwango cha usalama na uzima wa kiafya kwa wananchi wa nchi hiyo.

Tags