Feb 21, 2018 03:12 UTC
  • MSF: Waislamu wa Rohingya wangali wanamiminika Bangladesh

Jumuiya ya Madaktari Wasio na Mipaka (MSF) imetangaza kuwa, mamia ya wakimbizi wa jamii ya Waislamu wa Rohingya wanaokimbia ukatili na mauaji nchini Myanmar wangali wanamiminika katika nchi jirani ya Bangladesh na kwamba mgogoro wa Rohingya bado unaendelea.

Jumuiya ya Madaktari Wasio na Mipaka yenye makao makuu mjini Geneva imesema kuwa, wakimbizi hao wapya wamekabiliana na ukatili na manyanyaso wakiwa majumbani na vijijini kwao huko Myanmar na kwamba wamelazimika kukimbia kutokana na ukatili huo.

Taarifa hiyo ya MSF imetolewa sambamba na uamuzi uliochukuliwa na serikali ya Bangladesh wa kuanza kutekeleza mpango wa kuwarejesha wakimbizi wa Kiislamu wa jamii ya Rohingya nchini Myanmar.

Tarehe 23 Novemba serikali ya Bangladesh na Myanmar zilitia saini makubaliano ya kuwarejesha wakimbizi hao nchini kwao, suala ambalo limezusha hasira za taasisi na jumuiya nyingi za kutetea haki za binadamu.

Askari wa jeshi la Myanmar wakichoma vijiji vya Waislamu wa Rohingya

Maelfu ya Waislamu wa jamii ya Rohingya wameuawa nchini Myanmar kutokana na mashambulizi ya kikatili yanayofanywa na mabudha wenye misimamo mikali wakishirikiana na jeshi la nchi hiyo.

Wislamu zaidi la laki saba wa Rohingya wamekimbilia nchi jirani ya Bangladesh.  

Tags