Feb 24, 2018 14:18 UTC
  • Cuba na Venezuela Kuungana Kukabiliana na Chokochoko za Marekani

Harakati ya Urafiki na Mshikamano wa Cuba na Venezuela imesisitiza kuhusu muungano wa nchi hizo mbili katika kukabiliana na chokochoko za uingiliaji wa Marekani.

Kwa mujibu wa Shirika Rasmi la Habari la Cuba, Prensa Latina, siku ya Ijumaa, mjini Caracas, Venezuela kulifanyika kikao cha tatu cha Harakati ya Kitaifa ya Urafiki wa Cuba na Venezuela ambapo washiriki walijadili njia za kukabiliana na Marekani pamoja na waitifaki wake wa Magharibi.

Yhonny García Mratibu Mkuu wa Harakati ya Mshikamano wa Cuba na Venezuela amesema kikao hicho kimeangazia hatua zilizochukuliwa mwaka 2017 na kuandaa mikakati ya mwaka 2018.

García ameongeza kuwa, katika kikao hicho washiriki walijadili mzingiro wa kiuchumi, kibiashara na kifedha wa Marekani dhidi ya Cuba kwa zaidi ya nusu karne sasa na kusema hivi sasa njama kama hizo zimeanza kutekelezwa dhidi ya Venezuela.

Aidha amesema kikao cha Ijumaa likihudhuriwa na wawakilishi 12 wa nchi za Amerika ya Latini na pia wajumbe wa vyama kadhaa za kisiasa na kijamii.

Rais Maduro wa Venezuela

Washiriki wa kikao hicho walitangaza kuunga mkono hatua zilizochukuliwa na Rais Nicolas Maduro wa Venezuela katika kukabiliana na vikwazo vya upande mmoja vya Marekani dhidi ya Wavenezuela.

Naye Rogelio Polanco, Balozi wa Cuba nchini Venezuela akihutubu katika kikao hicho alisisitiza kuhusu ulazima wa umoja na mashikamano katika kukabiliana na ubeberu wa Marekani .

Harakati ya Urafiki na Mshikamano wa Cuba na Venezuela ilianzishwa mwaka 2003 na inajumuisha harakati na taasisi kadhaa za kijamii.

Tags