Rogozin: Russia ipo tayari kukabiliana na vikwazo
Naibu Waziri Mkuu wa Russia amesema kuwa Moscow ipo tayari kukabiliana na vikwazo vya Magharibi.
Dmitry Rogozin amesema kuwa sekta ya ulinzi na kijeshi ya Russia imestawi licha ya vikwazo hivyo vya Magharibi. Naibu Waziri Mkuu wa Russia ameongeza kuwa ni wazi kuwa vikwazo hivyo vya Magharibi ni radiamali ya adui mkongwe kwa juhudi zinazofanywa na Russia za kuwa huru katika matendo yake na kwamba jitihada hizo zitasita tu iwapo nchi hiyo itadhoofika tena.
Dimitry Rogozin amebainisha kuwa ni wazi kuwa vikwazo dhidi ya Russia ni fursa nzuri kwa ajili ya kutoa kipaumbele kwa hatua zinazochukuliwa na Russia katika uga wa kitaifa. Naibu Waziri Mkuu wa Russia amebainisha pia kwamba nchi hiyo ni ya pili baada ya Marekani kwa kuwa na soko kubwa la silaha kimataifa; ambapo mapato ya Russia kutokana na uuzaji wa silaha yamefikia zaidi ya dola bilioni 15 hivi sasa. Marekani na waitifaki wake wa Ulaya wameiwekea Russia vikwazo kwa kisingizio cha uingiliaji kati wa Moscow na kufuatia kushadidi hali ya mgogoro huko Ukraine na kuenea mapigano mashariki mwa nchi hiyo. Russia pia imejibu vikwazo hivyo vya Magharibi ambapo imeziwekea vikwazo Marekani na waitifaki wake hao.