Uturuki: Marekani isithubutu kutuwekea aina yoyote ya vikwazo, sisi ni marafiki
https://parstoday.ir/sw/news/world-i41475-uturuki_marekani_isithubutu_kutuwekea_aina_yoyote_ya_vikwazo_sisi_ni_marafiki
Serikali ya Uturuki kupitia Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi hiyo, imeitahadharisha Marekani juu ya kuiwekea vikwazo vya aina yoyote.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 10, 2018 23:57 UTC
  • Uturuki: Marekani isithubutu kutuwekea aina yoyote ya vikwazo, sisi ni marafiki

Serikali ya Uturuki kupitia Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi hiyo, imeitahadharisha Marekani juu ya kuiwekea vikwazo vya aina yoyote.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, Mevlüt Çavuşoğlu ametoa indhari hiyo akizungumza na mwandishi wa habari wa Ujerumani juu ya uwezekano wa serikali ya Ankara kuwekewa vikwazo na Marekani, na kusema kuwa kamwe Uturuki haitonyamazia kimya hatua hiyo na badala yake itatoa jibu kali dhidi ya Washington.

Mevlüt Çavuşoğlu, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki

Kadhalika Çavuşoğlu ameongeza kwamba, ni suala la kusikitisha kwamba baadhi ya nchi za Magharibi hadi sasa hazijafahamu ni namna gani zinatakiwa kuamiliana na nchi kama vile Uturuki. Amesisitiza kwamba, Marekani na nchi za Umoja wa Ulaya zinatakiwa zifahamu kwamba, Uturuki ni moja ya nchi washirika wakubwa. Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki ameelezea suala la kutolewa hukumu ya kifungo cha maisha kwa baadhi ya waandishi wa habari nchini humo na kusema kuwa, watu hao walihukumiwa adhabu hiyo baada ya kupatikana na hatia ya kuwa wanachama wa kundi la Fethullah Gülen, mtuhumiwa mkuu wa jaribio la mapinduzi ya kijeshi ya tarehe 15 Julai 2016 au kwa kuwa na mahusiano na kundi la Kikurdi pa PKK.