Putin apata ushindi wa kishindo katika uchaguzi wa rais Russia
Vladimir Putin amechaguliwa tena kuingoza Russia baada ya kupata ushindi wa kishindo katika uchaguzi uliofanyika jana.
Kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa na Tume Kuu ya Uchaguzi, baada ya kuhesabiwa asilimia 99 ya kura zote, Putin, wa chama cha Russia Iliyoungana (Yedinaya Rossiya ) amepata asilimia 76.64 au kura milioni 55.4 na hivyo ameibuka mshindi katika uchaguzi huo. Nafasi ya pili imechukuliwa na Pavel Grudinin wa Chama cha Kikomunisti ambaye alipata asilimia 11.82 ya kura sawa na kura milioni 8.54 huku nafasi ya tatu ikichukuliwa na Vladimir Zhirinovsky wa chama cha Liberal Democratic aliyepata asilimia 5/68 au kura milioni 4.1.

Punde baada ya matokeo ya awali kutangazwa, Putin amewahutubia wafuasi wake mjini Moscow na kuwashukuru kwa kumpigia kura. Putin alichaguliwa mara ya kwanza kuwa rais mwaka 2000 na kupata ushindi katika muhula wa pili baadaye. Kutokana na kuwa katiba haikumruhusu awanie urais zaidi ya mihula miwili mfululizo, hakuwania urais mwaka 2008 na badala yake aliteuliwa kuwa waziri mkuu. Baada ya hapo muhula wa urais uliongezwa kuwa miaka sita na Putin akagombea mwaka 2012 na kupata asilimia 63.6 ya kura. Kufuatia ushindi wa jana Putin anatazamiwa kuingoza Russia hadi mwaka 2024 wakati atatimiza umri wa miaka 72.