Maandamano Tel Aviv baada ya kuhani kuwatusi Waafrika kuwa ni nyani
Watu Zaidi ya 24,000, wengi wakiwa ni wahajiri, wameandamana katika mji mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel wakilaani kubaguliwa Waafrika.
Maandamano hayo yameitishwa siku chache baada ya kuhani mmoja wa Kizayuni kuwafananisha watu weusi wenye asili ya Afrika na nyani. Watetezi wa haki za binadamu wamesema matamshi yaliyotolewa hivi karibuni na Rabbi Yitzhak Yosef wa Israel ni ya kibaguzi na yasiyokubalika.
Aidha washiriki wa maandamano hayo wamelaani vikali mpango wa utawala haramu wa Israel wa kuwatimua wahajiri wa Kiafrika na kuwapeleka kwa lazima katika kambi maalumu zilizoko Rwanda na Uganda kuanzia Aprili Mosi. Karibu wahajiri 38,000 wa Kiafrika, wengi wakiwa ni Waeritrea na Wasudan wamepewa notisi ya kuwataka waondoke Israel au wakamatwe. Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel Benjamin Netanyahu amesema wahajiri wanaoingia katika utawala huo ni hatari zaidi ya magaidi. Mashirika ya kimataifa ya kutetea haki za binadamu yamelaani vikali kutimuliwa wahajiri hao, ambao wengi ni Mayahudi Waafrika.
Kwa miaka mingi utawala wa Kizayuni wa Israel umekuwa ukijaribu kuwavutia Mayahudi kutoka maeneo yote duniani kuhamia katika ardhi za Palestina zilizonyakuliwa kwa lengo la kubadilisha muundo wa kijamii katika ardhi hizo zinazokaliwa kwa mabavu.
Kutimuliwa wahajiri hao kumeibua maswali mengi kuhusu maana na lengo la utawala wa Israel, huku Mayahudi wengi Waafrika wakiamini kuwa wanabaguliwa kwa sababu ya rangi ya ngozi yao.