Ripoti: Facebook inahudumia malengo ya Israel
Wizara ya Sheria ya Israel imetangaza kuwa, idara inayosimamia mtandao wa kijamii wa Facebook ilikubali asilimia karibu 85 ya matakwa ya utawala huo haramu ya kuondolewa na kuzuiwa maelezo yanayohusiana na Wapalestina na jinsi wanavyokandamizwa katika kurasa za mtandao huo.
Taarifa hiyo ya Wizara ya Sheria ya Israel kuhusu Facebook imetolewa huku takwimu mpya zikionesha kuwa, wasimamizi wa Facebook wamezidisha kasi ya kufunga kurasa zote za watetezi na wapigania uhuru wa Wapalestina hususan baada ya Rais Donald Trump wa Marekani kuutangaza mji mtakatifu wa Baitul Muqaddas (Jerusalem) kuwa ni mji mkuu wa utawala haramu wa Israel.
Takwimu hizo zinaonesha kuwa, utawala haramu wa Isarel unafanya kazi na mitandao ya kijamii kupiga vita hata neno "Palestina" katika kurasa za mitandao hiyo na kwamba kila mtu anayetoa maelezo kuhusu mapambano ya ukombozi wa Palestina au kuzungumzia haki yake ya kupigania uhuru na ukombozi anafungiwa katika mitandao hiyo kwa kisingizio cha "kuchochea ugaidi".
Wakati huo huo idara ya Facebook haijachukua hatua yoyote dhidi ya maelfu ya kurasa za Kiisraeli zinazochochea ukatili, chuki na mauaji ya raia wasio na hatia wa Palestina.
Kwa sasa mtandao wa kijamii wa Facebook uko chini ya mashinikizo makali baada ya kukiri kwamba, ilifanya uzembe baada ya kubainika kuwa kampuni ya Uingereza Cambridge Analytica ilifanikiwa kudukua taarifa binafsi za mamilioni ya watumiaji wa Facbook kupitia progarmu maalumu ya utafiti ambayo ilipakuliwa na mamilioni ya watumiaji wa mtandao huo na kuchukua taarifa za watu wengi.