Lavrov: Russia itajibu ufidhuli wa nchi za Magharibi
https://parstoday.ir/sw/news/world-i42298-lavrov_russia_itajibu_ufidhuli_wa_nchi_za_magharibi
Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Russia amesema kuwa Moscow haitanyamaza kimya mbele ya hatua ya nchi za Magharibi ya kuwafukuza wanadiplomasia wa nchi hiyo.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Mar 27, 2018 22:41 UTC
  • Lavrov: Russia itajibu ufidhuli wa nchi za Magharibi

Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Russia amesema kuwa Moscow haitanyamaza kimya mbele ya hatua ya nchi za Magharibi ya kuwafukuza wanadiplomasia wa nchi hiyo.

Sergei Lavrov amewaambia waandishi habari mapema leo kwamba, hatua ya baadhi ya nchi kuomba radhi kutokana na kuwafukuza wanadiplomasia wa Russia ni kielelezo kwamba suala hilo limefanyika kwa mashinikizo makubwa ya Marekani ambayo ndio wenzo unaotumiwa na Washington katika medani ya kimataifa.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amesema kuwa, kufukuzwa wanadiplomasia wa Russia katika nchi kadhaa za Magharibi ni ishara kwamba, nchi zinazojitegemea dunia ni chache sana. 

Lavrov pia ameashiria matamshi yaliyotolewa na Waziri Mkuu wa Uingereza, Theresa May kuhusu kadhia ya kupewa sumu jasusi wa zamani wa Russia, Sergei Skripal na kusema: Matamshi hayo ya May yamedunisha na kudharau mahakama za Uingereza. 

Russia imeapa kujibu hatua ya nchi za Magharibi

Ni vyema kuashiria hapa kwamba nchi 14 wanachama wa Umoja wa Ulaya, Marekani, Canada, Ukraine na Australia zimewafukuza makumi ya wanadiplomasia wa Russia zikionesha mshikamano wao na Uingereza baada ya London kudai kuwa Russia ilihusika na jaribio la kutaka kumuua jasusi wa zamani wa nchi hiyo, Sergei Skripal na binti yake, Yulia katika eneo la Salisbury huko kusini mwa London. Russia imekanusha vikali madai hayo.