Viongozi wa Korea mbili kukutana mwishoni mwa mwezi ujao
Korea Kaskazini na Korea Kusini zimetangaza kuwa viongozi wa nchi mbili hizo jirani watakutana na kufanya mazungumzo tarehe 27 mwezi Aprili mwaka huu.
Tarehe hiyo imetangazwa leo Alkhamisi baada ya kufanyika mazungumzo ya ngazi ya juu kati ya Korea mbili hizo katika kijiji cha Panmunjom kilichoko katika mpaka wa nchi hizo za Peninsula ya Korea.
Waziri wa Korea Kusini wa Uunganishaji wa Korea mbili ambaye alikuwa anaongoza ujumbe wa ngazi ya juu wa Seoul amesema, "Mkutano wa Aprili utakuwa ni kufunguliwa kwa ukurasa mpya na kuanza safari ya kuleta amani katika Peninsula ya Korea, kuimarisha uhusiano wa pande mbili, na kufanikisha mchakato wa kuwa na eneo la Korea lisilo na silaha za nyuklia."
Naye Ri Son-gwon, mkuu wa ujumbe wa ngazi ya juu wa Korea Kaskazini amesema mambo mengi yamekuwa yakifanyika nyuma ya pazia ndani ya siku 80 zilizopita, kuhakikisha kuwa wanafikia hatua iliyofikiwa leo.
Mazungumzo hayo ya leo Alkhamisi yamefanyika baada ya Kim Jong-un, Kiongozi wa Korea Kaskazini kukutana na Rais Xi Jinping wa China mjini Beijing na kuzungumzia masuala ya uhusiano wa nchi mbili na kadhalika mgogoro na taharuki katika Peninsula ya Korea.
Mahusiano kati ya Pyongyang na Seoul yamekuwa yakiboreka tangu kulipojiri mazungumzo ya pande mbili kwa ajili ya kuishawishi Korea Kaskazini ishiriki katika michuano ya olimpiki katika msimu wa baridi kali nchini Korea Kusini.