Kukiri Ujerumani nafasi muhimu ya Russia ulimwenguni
https://parstoday.ir/sw/news/world-i42538-kukiri_ujerumani_nafasi_muhimu_ya_russia_ulimwenguni
Heiko Maas, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, amesema kuwa nchi yake inakaribisha mazungumzo na Russia kwa ajili ya kukomesha mgogoro uliojitokeza hivi sasa baina ya Moscow na nchi za Magharibi zikiongozwa na Uingereza.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 02, 2018 09:32 UTC
  • Kukiri Ujerumani nafasi muhimu ya Russia ulimwenguni

Heiko Maas, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, amesema kuwa nchi yake inakaribisha mazungumzo na Russia kwa ajili ya kukomesha mgogoro uliojitokeza hivi sasa baina ya Moscow na nchi za Magharibi zikiongozwa na Uingereza.

Hata hivyo, waziri huyo wa mambo ya nje wa Ujerumani amedai kuwa, mienendo ya Russia katika miaka ya hivi karibuni imeondoa hali ya kuaminiana lakini pamoja na hayo, wao wako tayari kufanya mazungumzo na kwamba inawezakana kujenga hali ya kuaminiania hatua kwa hatua iwapo Russia itakuwa tayari kufanya hivyo. Amesema: Sisi tunaiangalia Russia kama mshirika wa kutatua matatizo ya kieneo na vile vile katika suala la upokonyaji silaha. Bali tunaihitajia Russia kwani ni moja ya nguzo muhimu katika masuala mengi.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Haiko Maas

 

Kukiri huko waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani ambayo ni moja ya nchi muhimu katika Umoja wa Ulaya na ambayo pia ina nafasi muhimu na ya kimsingi ndani ya umoja huyo na ndani ya NATO, kunaonesha kubadilika misimamo ya kambi ya Marekani kuhusu nafasi muhimu isiyo na mbadala ya Russia katika matukio ya hivi sasa duniani. Lakini si Ujerumaini pekee inayoiangalia Russia kwa jicho hilo, bali nchi nyingine kadhaa za Ulaya nazo zinakiri nafasi ya kimsingi ya Russia katika utatuzi wa masuala ya Ulaya na ya kimataifa. Wazungu wanaelewa vyema kwamba hawawezi kutatua migogoro ya bara hilo kama ule wa Ukraine bila ya kuishirikisha kikamilifu Russia. Fauka ya hayo, Russia inahesabiwa kuwa ni dola kubwa la nyuklia duniani pamoja na Marekani na kama nchi za Ulaya zitaipuuza Moscow basi zitashindwa kudhamini usalama wa bara hilo hasa kwa kuzingatia kuwa Russia ni mawanachama katika mikataba muhimu ya nyuklia kama ule wa Intermediate-Range Nuclear Forces Treaty (INF) na ule wa New START. 

Hata hivyo, kinyume na matakwa ya Wazungu wa Ulaya, tunaona kuwa mshirika wa nchi za bara hilo katika janibu ya pili ya Bahari ya Atlantiki yaani Marekani anazingatia zaidi siasa za kujinufaisha binafsi katika kipindi hiki cha baada ya vita baridi na anajifanya polisi wa dunia na kudharau nafasi ya nchi zote nyingine duniani. Marekani inadharau pia nafasi ya taasisi za kimataifa kama Umoja wa Marekani katika utatuzi wa masuala ya kimataifa. Baya zaidi ni kwamba serikali ya hivi sasa ya Donald Trump huko Marekani imezidi kudharau nafasi ya taasisi na madola mengine duniani kwa kaulimbiu yake kuu ya "Marekani Kwanza" na imekuwa ikichukua hatua mbalimbali zenye madhara kwa nchi nyingine kama ile sheria ya kuiwekea vikwazo Russia inayojulikana kwa jina maarufu la sheria ya CATSA ambayo ina madhara ya moja kwa moja kwa nchi za Ulaya. 

Profesa Vladimir Zakharova

 

Msomi wa hisabati wa nchini Russia, Profesa Vladimir Zakharov anasema: Kwa hatua zake mpya ikiwa ni pamoja na kupitisha sheria inayojulikana kwa jina la CATSA, Marekani kwa hakika imezionesha nchi za Ulaya kuwa inaweza kufanya chochote bila ya kuzishirikisha na imekusudia kutoa pigo kwa nchi hizo kupitia sheria hiyo.

Hii ni katika hali ambayo, mara kwa mara Russia imekuwa ikitangaza wazi kuwa inapinga utawala wa kambi moja duniani unaopiganiwa na dola la kibeberu la Marekani. Hata hivyo katika kipindi chote hiki cha baada ya vita baridi, Marekani imekuwa ikichukua hatua mbalimbali za kuonesha kwamba duniani hivi sasa kuna kambi moja tu yenye nguvu nayo ni Marekani ingawa uhalisia wa mambo unaonesha kinyume chake kabisa. Matukio mbalimbali kama ya Ukraine, Iraq na Syria yamethibitisha kuwa njozi za Marekani za kutaka kuwa dola pekee lenye nguvu duniani ni ndoto za mchana ambazo kamwe haziwezi kuagulika. Mara kwa mara Rais Vladimir Putin wa Russia amekuwa akisema kwamba, siasa za kuwa na kambi moja tu duniani inayoongozwa na Marekani haziwezi kabisa kukubaliwa na Moscow. Ndio maana kwa muda mrefu sasa Russia imekuwa ikichukua hatua za kuzuia jambo hilo, na kitendo cha Ujerumani cha kukiri hadharani nafasi muhimu ya Moscow katika matukio ya dunia, ni uthibitisho wa kufeli siasa za kuifanya dunia itawaliwe na kambi moja inayoongozwa na Marekani.