Apr 14, 2018 07:06 UTC
  • Jeshi la Myanmar lawekwa katika orodha nyeusi ya UN

Ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa imeliweka jeshi la Myanmar katika orodha nyeusi ya umoja huo, kutokana na jinai za ubakaji zilizofanywa na askari wa nchi hiyo dhidi ya Waislamu wa Rohingya.

Nakala ya ripoti hiyo ya Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa Baraza la Usalama la umoja huo na iliyoonekana jana Ijumaa na shirika la habari la Associated Press imefichua kuwa, aghalabu ya Waislamu laki saba wa Rohingya waliokimbilia nchini Bangladesh wana majeraha ya kisaikolojia na makovu kwenye miili yao yalitokana na jinai za ubakaji walizofanyiwa na wanajeshi katili wa Myanmar.

Guterres amesema kwenye ripoti hiyo ya kwanza kabisa kuilaani wazi wazi serikali ya Myanmar kwamba, "Jinai hizo za ubakaji zilifanywa na kikosi cha Jeshi la Myanmar kinachojulikana kama Tatmadaw, katika operesheni zilizokusudia kuwadhalilisha, kuwatesa na kuiadhibu jamii nzima ya Warohingya."

Hivi karibuni, shirika la kutetea haki za binadmau la Human Rights Watch (HRW) lilisema jeshi la Myanmar linawaua kiholela na kuwabaka wanawake Waislamu wa jamii ya Rohingya magharibi mwa nchi hiyo.

Wanawake Waislamu wa Rohingya

 

Maelfu ya Waislamu wa kabila la Rohingya nchini Myanmar wameuawa na maelfu ya wengine kujeruhiwa tangu kuanza wimbi jipya la mashambulizi ya jeshi na Mabudha wenye misimamo mikali katika mkoa wa Rakhine magharibi mwa nchi nchi hiyo tangu tarehe 25 Agosti mwaka huu hadi sasa. 

Mauaji hayo ya umati dhidi ya Waislamu nchini Myanmar yamepelekea zaidi ya nusu milioni kati yao kukimbilia hifadhi katika nchi jirani ya Bangladesh.

Tags