Hatua zenye kukinzana za Uingereza kuhusu makubaliano ya JCPOA
Ikiwa imekaribia muda wa kuchukuliwa uamuzi na Rais wa Marekani kuhusu makubaliano ya nyuklia yaliyofikiwa kati ya kundi la 5+1 na Iran, juhudi za kimataifa pia zimeongezeka ili kuishaiwishi nchi hiyo itekeleze ahadi na majukumu yake kimataifa.
Baada ya safari ya Rais wa Ufaransa na Kansela wa Ujerumani mjini Washington, Boris Johnson Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza pia leo Jumapili anaelekea mjini humo kwa lengo la kumshawishi Rais Donald Trump asalie kwenye makubaliano hayo ya nyuklia. Rais wa Marekani anapasa mara moja kila baada ya siku 120 arefushe muda wa usimamishaji vikwazo vya nyuklia dhidi ya Iran.
Kujizuia kuiwekea Iran vikwazo vipya vya nyuklia ni moja ya wajibu unaopasa kutekelezwa na Marekani katika fremu ya makubaliano hayo. Pamoja na hilo, Trump mwezi Januari uliopita alitishia kuwa atajizuia kuongeza muda wa usitishaji vikwazo dhidi ya Iran iwapo nchi za Ulaya hazitakubali masharti ya Marekani. Kuzuia miradi ya makombora ya Iran, kupanua ukaguzi na kubadilishwa jedwali la muda wa makubaliano ya JCPOA ni miongoni mwa masharti yaliyotajwa na Trump; ambayo yote yanakinzana kikamilifu na yale yaliyoafikiwa na serikali ya Marekani katika mazungumzo ya nyuklia.
Kwa kuzingatia muamala kama huo Uingereza ikiwa moja ya nchi tatu za Ulaya zilizoshiriki katika mazungumzo ya nyuklia, katika siku za hivi karibuni imeonekana kuzidisha jitihada zake ili kumridhisha Rais wa Marekani. Hata hivyo London imechagua njia kinzani ili kufanikisha lengo hilo. Kwa upande mmoja, Uingereza sawa kabisa na aghalabu ya nchi nyingine duniani inasisitiza kuendelezwa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na kusalia Marekani kwenye makubaliano hayo; na katika upande mwingine ili kuweza kumridhisha Trump, nchi hiyo imesema kuwa kuna udharura wa kufanyika mazungumzo ya ziada kuhusu makubaliano hayo au kuhusiana na miradi ya makombora na harakati za kieneo za Iran. Kitendo cha Uingereza, Ufaransa pamoja na Ujerumani cha kutuma jumbe zenye utata na zinazokinzana; nchi ambazo zilishiriki katika mazungumzo ya nyuklia na Iran, kinatoa msukumo na kumshajiisha Rais wa Marekani kuvuruga makubaliano hayo ya nyuklia. Katika hali ambayo makubaliano hayo yanayojulikana kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA) yanatambulika kama waraka ulio wazi na usio na utata wowote, yameainisha waziwazi majukumu na wajibu wote wa nchi na taasisi za kimataifa kuhusiana na miradi ya nyuklia ya Iran. Kwa mujibu wa mchakato uliotabiriwa katika mchakato huo, Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia (IAEA) umethibitisha katika ripoti zake 11 za msimu kwamba Iran imetekeleza kikamilifu majukumu yake. Hii ni katika hali ambayo upande wa Marekani umekiuka ahadi na majukumu yake kwa kuendeleza vitisho dhidi ya nchi mbalimbali na mashirika binafsi yaliyoonyesha hamu ya kushirikiana kiuchumi na Iran.
Edwin Samuel msemaji wa serikali ya Uingereza anasema: Kwa mtazamo wa London, kuvunjwa makubaliano ya JCPOA si kwa maslahi ya pande husika katika mapatano hayo ya kimataifa ikiwemo Marekani.
Kuendelea mchakato huu si tu kuwa kutasambaratisha makubaliano hayo ya nyuklia na Iran, bali kutakuwa na athari hasi pia kwa uhusiano wa Trans-Atlantic. Wakati huo huo mashirika ya Ulaya pia yatadhurika pakubwa iwapo Marekani itarejesha vikwazo vyake hivyo maarufu kama vikwazo vya upili. Hii ni kwa sababu mashirika hayo yamewekeza pakubwa nchini Iran miaka mitatu baada ya kutekelezwa makubaliano ya JCPOA sambamba na kuanzishwa fursa nzuri kwa ajili ya wawekezaji wa sekta ya uchumi kutoka nchi za Ulaya. Kwa msingi huo vizuizi na mikwamo inayotekelezwa na Marekani katika kuendelezwa ushirikiano huu vitasababisha kupotea kwa fursa nyingi za ajira na wawekezaji kutoka Ulaya. Ni kwa sababu hiyo pia ndipo katika wiki za hivi karibuni viongozi wa nchi za Ulaya wameonekana kuzidisha juhudi ili kulinda makubaliano ya JCPOA. Wakati huo huo mtazamo wa kutaka makuu na kutarajia makubwa wa Marekani kuhusu masuala mbalimbali ya kimataifa na ubinafsi wa Trump mkabala na makubaliano hayo, yote hayo yameyatumbukiza hatarini maslahi ya pande zote wakiwemo washirika wa Ulaya wa Washington.