Wamarekani wengi wanataka US ibakie kwenye JCPOA
https://parstoday.ir/sw/news/world-i44218-wamarekani_wengi_wanataka_us_ibakie_kwenye_jcpoa
Utafiti wa maoni wa hivi punde unaonyesha kuwa thuluthi mbili ya wananchi wa Marekani wanaamini kuwa nchi yao haipaswi kujiondoa kwenye makubaliano ya nyuklia ya Iran, huku yakiwa yamesalia masaa machache kabla Rais Donald Trump atangaze iwapo Washington itajiondoa kwenye mapatano hayo ya kimataifa au la.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 08, 2018 12:28 UTC
  • Wamarekani wengi wanataka US ibakie kwenye JCPOA

Utafiti wa maoni wa hivi punde unaonyesha kuwa thuluthi mbili ya wananchi wa Marekani wanaamini kuwa nchi yao haipaswi kujiondoa kwenye makubaliano ya nyuklia ya Iran, huku yakiwa yamesalia masaa machache kabla Rais Donald Trump atangaze iwapo Washington itajiondoa kwenye mapatano hayo ya kimataifa au la.

Utafiti huo uliofanywa na Kituo cha Utafiti cha SSRS kwa niaba ya shirika la habari la CNN umeonyesha kuwa, asilimia 63 ya Wamarekani wanaamini kuwa Trump hapaswi kuiondoa nchi hiyo kwenye makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, huku asilimia 29 tu ikiunga mkono azma hiyo ya Trump.

Utafiti huo umebainisha kuwa, asilimia 51 ya wafuasi wa chama cha Republican cha Trump wanaunga mkono hatua ya Marekani kujiondoa kwenye makubaliano hayo yaliyoanza kutekelezwa Januari mwaka 2016, huku asilimia 46 miongoni mwao wakiunga mkono uongozi wa Trump.

Rais Donald Trump

Wiki iliyopita, utafiti mwingine uliofanywa na shirika la utafiti la Morning Consultant/Politico ulionyesha kuwa, asilimia 56 ya Wamarekani wanaunga mkono makubaliano hayo ya nyuklia kati ya Iran na nchi wananchama wa Kundi la 5+1, huku asilimia 26 tu wakiyapinga.    

Trump ambaye amekuwa akiyaponda makubaliano hayo na kuyataja kuwa mapatano mabaya zaidi katika historia ya Marekani anatazamiwa hii leo kuchukua uamuzi wa ama kubakia kwenye makubaliano hayo au kujitoa.