Kujitoa katika JCPOA au kujenga uadui na Jamii ya Kimataifa
Hatimaye Marekani imejitoa kwenye makubaliano ya pamoja ya nchi saba ukiwemo Umoja wa Ulaya, ambayo utekelezaji wake ulidhaminiwa na azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Katika hotuba iliyojaa lugha ya matusi na vitisho dhidi ya taifa la Iran, na baada ya miezi 17 ya kutoa vitisho na masharti haya na yale, hatimaye Donald Trump ametangaza uamuzi wa kujitoa Marekani katika makubaliano ya nyuklia na Iran. Ukweli ni kwamba kwa uamuzi wake huo, Trump amethibitisha rasmi mwenendo wa kuhalifu ahadi na kukiuka makubaliano ambao Marekani iliuanzisha muda mrefu nyuma kuhusiana na makubaliano ya nyuklia.
Makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, tab'an si mhanga wa kwanza wa uadui wa Marekani dhidi ya Iran na uchukuaji misimamo ya upande mmoja na ya mihemko ya mrengo tawala wenye misimamo ya utaifa wa kufurutu mpaka nchini Marekani katika kuamiliana na Jamii ya Kimataifa. Kuanzia siku ya kwanza tu ya baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, yaani mnamo mwezi Februari mwaka 1979, wananchi wa Iran walianza kukabiliwa na uadui wa Marekani; na mifano kadhaa ya uadui huo ukiwemo wa kumuunga mkono Saddam katika vita vya miaka minane dhidi ya Iran na kuitungua ndege ya abiria ya Iran katika anga ya maji ya Ghuba ya Uajemi zingali kwenye kumbukumbu za historia za wananchi hao.
Lakini kabla JCPOA pia kuna mikataba mingine kadhaa ambayo imefanywa mhanga na serikali zilizopita na ya sasa ya Marekani, ukiwemo mkataba wa mabadiliko ya tabianchi wa Kyoto wakati wa serikali ya Bill Clinton, mkataba wa kupiga marufuku uundaji makombora ya kutungulia makombora katika serikali ya George W. Bush na hatimaye ukiukaji kadhaa wa makubaliano unaofanywa na serikali ya Trump.
Katika miezi 15 iliyopita Marekani imejitoa kwenye mkataba wa tabianchi wa Paris na mkataba wa kibiashara wa Trans-Pasific. Kama vile haitoshi imeamua pia kujitoa kwenye Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), na katika hatua inayokinzana na takwa la Jamii ya Kimataifa imeitambua Quds kuwa mji mkuu wa utawala haramu wa Kizayuni wa Israel.
Hata hivyo kila moja ya mielekeo hiyo ya kujichukulia uamuzi wa upande mmoja ya serikali ya Marekani imekabiliwa na hasira na manung'uniko ya hata waitifaki wa karibu wa Washington.
Kwa kutangaza rasmi kujitoa kwenye JCPOA, sasa Trump ameondoa utata uliokuwepo kuhusiana na watekelezaji wa makubaliano hayo. Kwa maana kwamba, kuanzia sasa makubaliano ya JCPOA yatakuwa ni baina ya Iran na nchi tano pamoja na Umoja wa Ulaya. Nchi zilizosalia katika makubaliano hayo ya Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji zimechukua dhima na kutoa ahadi ya kuendelea kutekeleza majukumu yao na kufidia hasara iliyosababishwa na Marekani. Jukumu hilo linazielekea zaidi nchi za Umoja wa Ulaya ambazo zitapaswa kuonyesha na kuthibitisha kivitendo kama zinaheshimu misingi yao ya kisiasa na kimaadili au mwishowe zitakuja kupiga magoti na kusalimu amri kwa matakwa ya mrengo wenye misimamo mikali zaidi dhidi ya juhudi za ushirikiano wa pamoja kimataifa.
Miaka 15 nyuma, msimamo unaofanana na huu uliochukuliwa sasa na Washington, ulichukuliwa kuhusiana na makubaliano ya nyuklia yaliyofikiwa kati ya Iran na nchi tatu za Troika ya Ulaya, yaani Uingereza, Ujerumani na Ufaransa na kupelekea kubadilika na kupanuliwa kwa kasi shughuli za nyuklia za Iran kiubora na kiidadi; kiasi kwamba wakati Marekani ilipojiunga na meza ya mazungumzo ya nyuklia, sentrifuji au mashinepewa za Iran ambazo hapo kabla idadi yake haikuzidi mia kadhaa tu zilifikia elfu ishirini. Kwa muktadha huo, haitokuwa baidi kwa hali hiyo kukaririwa na kurudiwa tena katika siku za usoni. Ni kama alivyoeleza Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika hotuba aliyotoa mara baada ya Marekani kutangaza uamuzi wa kujitoa kwenye JCPOA.
Rais Hassan Rouhani alisema: "Nimeshaliamuru Shirika la Nishati ya Atomiki lijiweke tayari kuchukua hatua zinazotakiwa, ili pale itakapohitajika tuweze kufanya urutubishaji wa kiviwanda usio na mpaka".
Uamuzi huo ndio ile ahadi ambayo Iran ilitoa kuhusu majuto ya kihistoria itakayopata Washington.../