Taarifa ya Troika ya Ulaya yaunga mkono kulindwa makubaliano ya JCPOA
Wakuu wa Ufaransa, Ujerumani na Uingreza baada ya kufanya kikao chao cha pande tatu katika mji mkuu wa Bulgaria, Sophia kwa mara nyingine tena wametaka kulindwa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA kwa hali zote.
Bi Theresa May Waziri Mkuu wa Uingereza, Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa na Kansela wa Ujerumani bi Angela Merkel wamesisitiza leo kwenye taarifa yao ya pamoja kwamba pande zote husika katika makubaliano hayo ya nyuklia zinapasa kufungamana na kuheshimu masharti yote ya makubaliano hayo.
Ufaransa, Uingereza na Ujerumani zimeitaka Iran iendelee kutekeleza majukumu yake kuhusiana na makubaliano hayo na kusisitiza kuhusu azma yao thabiti ya kuyalinda makubaliano hayo ya nyuklia. Wakuu hao wa Ujerumani, Ufaransa na Uingereza sambamba na kusisitiza kulindwa makubaliano ya JCPOA wamezungumzia pia suala la kukabiliana na miradi ya makombora na harakati za Iran katika eneo. Nchi hizo za Ulaya zinafanya jitihada za kuyalinda makubaliano hayo yaliyofikiwa kati ya kundi la 5+1 na Iran kufuatia Marekani kujitoa katika makubaliano hayo tarehe nane mwezi huu. Baada ya kutangaza kujitoa Marekani katika JCPOA, Rais Donald Trump alisaini dikrii ya kurejeshwa vikwazo dhidi ya Iran na kuzitahadharisha nchi za Ulaya kuhusu kufanya biashara na Iran. Iran kwa upande wake imetangaza kuwa itaendelea kubaki katika makubaliano ya JCPOA iwapo maslahi yake yatadhaminiwa.