Mogherini: Kulindwa JCPOA kuna umuhimu wa kiusalama kwa Ulaya
https://parstoday.ir/sw/news/world-i45106-mogherini_kulindwa_jcpoa_kuna_umuhimu_wa_kiusalama_kwa_ulaya
Mkuu wa Siasa za Kigeni wa Umoja wa Ulaya amesema kuwa, kulindwa mapatano ya nyuklia ya JCPOA kuna umuhimu wa kiusalama kwa bara Ulaya.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 28, 2018 21:15 UTC
  • Mogherini: Kulindwa JCPOA kuna umuhimu wa kiusalama kwa Ulaya

Mkuu wa Siasa za Kigeni wa Umoja wa Ulaya amesema kuwa, kulindwa mapatano ya nyuklia ya JCPOA kuna umuhimu wa kiusalama kwa bara Ulaya.

Federica Mogherini amesema hayo usiku wa kuamkia leo (Jumatatu) baada ya kumalizika kikao cha mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya mjini Brussels, Ubelgiji, na kuongeza kuwa, umoja huo hivi sasa unajadili njia za kuipa Iran vivutio vya kiuchumi ili kuyalinda mapatano hayo.

Amesema, kulindwa JCPOA hakuna manufaa ya kiuchumi tu kwa Umoja wa Ulaya, bali umoja huo unayahitajia mapatano hayo katika masuala yake ya kiusalama.

Pande zilizofanikisha kufikiwa mapatano ya nyuklia ya JCPOA

 

Amma kuhusiana na kikao cha jana Jumatatu cha mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya, Mogherini amesema, baadhi ya nchi wanachama wa umoja huo zimetoa mapendekezo maalumu ya kuweza kulindwa miamala ya kibiashara baina ya Iran na Umoja wa Ulaya.

Kabla ya hapo, mkuu huyo wa sera za kigeni za Umoja wa Ulaya alikuwa amesema katika ufunguzi wa kikao hicho cha jana kuwa, ajenda ya awali kabisa na muhimu zaidi ya kikao hicho cha Baraza la Mawaziri wa Mambo ya Nje la Umoja wa Ulaya ni kulindwa JCPOA.

Itakumbukwa kuwa Jumanne usiku tarehe 8 Mei, 2018, rais wa Marekani, Donald Trump alitangaza kuitoa nchi yake kwenye mapatano ya JCPOA licha ya kwamba Washington ilikuwa mstari wa mbele kuyafanikisha wakati wa urais wa Barack Obama.