Trump na Shinzō Abe wapanga kuibana zaidi Korea Kaskazini
https://parstoday.ir/sw/news/world-i45114-trump_na_shinzō_abe_wapanga_kuibana_zaidi_korea_kaskazini
Rais Donald Trump wa Marekani na Shinzō Abe, Waziri Mkuu wa Japan wamekubaliana kuhakikisha wanailazimisha Korea Kaskazin iachane na silaha zake za nyuklia na makombora ya balestiki.
(last modified 2026-04-19T09:26:01+00:00 )
May 29, 2018 02:48 UTC
  • Trump na Shinzō Abe wapanga kuibana zaidi Korea Kaskazini

Rais Donald Trump wa Marekani na Shinzō Abe, Waziri Mkuu wa Japan wamekubaliana kuhakikisha wanailazimisha Korea Kaskazin iachane na silaha zake za nyuklia na makombora ya balestiki.

Taarifa iliyotolewa na ikulu ya Marekani White House imesema kuwa, Trump na Abe walijadiliana masuala hayo jana Jumatatu kupitia mazungumzo ya simu ambapo walikubaliana kutoiruhusu Korea Kaskazini kuwa na silaha hizo na badala yake kuhakikisha inaziangamiza.

Kim Jong-un, Kiongozi wa Korea Kaskazini

Aidha taarifa hiyo imeongeza kwamba, viongozi hao wa Marekani na Japan walizungumzia matukio ya hivi karibuni nchini Korea Kaskazini sambamba na kusisitizia umuhimu wa kutokomezwa kikamilifu miradi ya nyuklia, silaha za kemikali, silaha za kibaiolojia na makombora ya balestiki ya taifa hilo. Kadhalika pande mbili zimekubaliana kuendeleza ushirikiano wao kabla ya kufanyika kikao tarajiwa kati ya Rais Donald Trump na Kim Jong-un.

Baadhi ya makombora ya Korea Kaskazini yanayozinyima usingizi Japan na Marekani

Hayo yanajiri katika hali ambayo wiki iliyopita na katika hatua ya ghafla Trump alitangaza kufutilia mbali mkutano uliokuwa umepangwa kufanyika tarehe 12 Juni nchini Singapore kati yake na kiongozi huyo wa Korea Kaskazini huku duru za ikulu ya White House zikifichua kuwa, alilitaka jeshi la nMarekani kujiweka tayari kwa ajili ya kukabiliana na Korea Kaskazini. Weledi wa mambo wanatilishia shaka iwapo Marekani anaweza kuikinasha serikali ya Pyongyang kutokomeza silaha zake ilizozipata kwa juhudi kubwa.