Russia: Marekani imejitoa kwenye JCPOA ili ikabiliane pande zote na Iran
https://parstoday.ir/sw/news/world-i45202-russia_marekani_imejitoa_kwenye_jcpoa_ili_ikabiliane_pande_zote_na_iran
Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amesema Marekani imeamua kujitoa kwenye makubaliano ya nyuklia ya Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji JCPOA kwa sababu inataka kukabiliana pande zote na Iran.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 30, 2018 23:10 UTC
  • Russia: Marekani imejitoa kwenye JCPOA ili ikabiliane pande zote na Iran

Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amesema Marekani imeamua kujitoa kwenye makubaliano ya nyuklia ya Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji JCPOA kwa sababu inataka kukabiliana pande zote na Iran.

Sergei Lavrov ameyasema hayo kwenye kongamano la kila mwaka la kimataifa la Primakov Readings lililofanyika katika mji mkuu wa Russia, Moscow na kubainisha kuwa, wakati Marekani ilipojitoa kwenye makubaliano ya JCPOA ilichagua kufanya hivyo kwa lengo la kukabiliana pande zote na Iran.

Lavrov ameongeza kuwa kuna mambo kadhaa yanayoathiri sera za nje za Marekani, ambazo mara zote huwa hazina muelekeo wa aina moja na mara nyingi huwa zina migongano.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amefafanua kuwa Marekani imeamua kutekeleza mkakati wenye lengo la kuitenga Iran kwa tamaa kwamba Tehran itapanga sera zake kwa namna itakayoridhi na kuendana na mkakati huo.

Iran na nchi sita kubwa duniani pamoja na Umoja wa Ulaya zilifikia makubaliano ya nyuklia ya JCPOA ambayo Marekani imejitoa kuthibitisha kuwa si nchi ya kuaminika kimataifa

Lavrov ametahadharisha kuwa lugha ya ubabe na vitisho haiwezi kufanikiwa kutatua masuala ya kimataifa wala kuwa na tija.

Aidha ameishauri Marekani ichukue hatua ya kuanzisha mazungumzo na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Primakov Readings ni kongamano la kimataifa linalofanyika kila mwaka nchini Russia kwa lengo la kuzungumzia masuala ya ulimwengu, siasa za kimataifa na usalama kwa kuhudhuriwa na wataalamu, wanadiplomasia na wanasiasa mbalimbali waandamizi.../