Fox News: Trump na kiongozi wa Korea Kaskazini ni madikteta
Televisheni ya wahafidhina wa Marekani ya Fox News ambayo ina uhusiano wa karibu sana na serikali ya nchi hiyo imeibua gumzo na mijadala baada ya kusema kuwa Rais Donald Trump na kiongozi wa Korea Kaskazini ni madikteta.
Fox News ilimtaja Trump kama dikteta hapo jana Jumapili katika kipindi cha Fox&Friends ambacho kinapendwa sana na Trump, wakati mtangazaji wa kanali hiyo na aliyekuwa Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Ikulu ya White House, Anthony Scaramucci walipokuwa wakijadili mkutano kati ya Trump na Kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong-un.
Mwenyeji wa kipindi hicho, Abby Huntsman, wakati akimtaka Scaramucci azungumzie mkutano huo wa Singapore, alisikika akisema, "Mbali na chochote kitakachofanyika katika mkutano huo wa madikteta wawili, lakini tunachoshuhudia hivi sasa ni historia."
Hata hivyo mtangazaji huyo ambaye ni binti ya balozi wa Marekani nchini Russia baadaye aliomba radhi na kudai kuwa hakukusudia kuwaita viongozi hao madikteta, bali ulimi uliteleza.
Suala hilo limeibua mijadala katika mitandao ya kijamii, ambapo baadhi ya watumiaji wa mtandao wa Twitter wanasema hatimaye Fox News imetangaza jambo lenye ukweli ndani yake kwa mara ya kwanza.
Tayari Kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong-un na Rais Donald Trump wa Marekani wamewasili nchini Singapore kwa ajili ya mkutano wao utakaofanyika hapo kesho, katika kisiwa cha Sentosa.