Croatia yaidhalilisha Argentina Kombe la Dunia Russia
https://parstoday.ir/sw/news/world-i46162-croatia_yaidhalilisha_argentina_kombe_la_dunia_russia
Timu ya taifa ya soka ya Croatia jana usiku iliidhalilisha Argentina na nyota wake mkubwa, Lionel Messi, baada ya kuichabanga magoli matatu kwa sifuri katika uwanja wa Nizhny Novgorod.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Jun 22, 2018 00:21 UTC
  • Croatia yaidhalilisha Argentina Kombe la Dunia Russia

Timu ya taifa ya soka ya Croatia jana usiku iliidhalilisha Argentina na nyota wake mkubwa, Lionel Messi, baada ya kuichabanga magoli matatu kwa sifuri katika uwanja wa Nizhny Novgorod.

Matokeo hayo yameipatia timu ya taifa ya Croatia tiketi ya kuingia duru ya pili ya mashindano hayo yanayoendelea nchini Russia. Hii ni mara ya kwanza wa timu ya taifa ya soka ya Croatia kufanikiwa kuingia duru ya pili ya Kombe la Dunia katika kipindi cha miaka 20 iliyopita.

Kipigo hicho cha mabao matatu kwa nunge kimeiweka timu iliyojaa nyota lakini butu ya Argentina katika hatari ya kutupwa nje ya mashindano ya Kombe la Dunia. Croatia inaongoza kundi D kwa kuwa na pointi sita huku Argentina ikiwa na pointi moja tu baada ya kulazimishwa sare ya bao moja kwa moja katika mechi yake ya kwanza na Iceland.

Timu nyingine mbili za kundi hilo yaani Nigeria na Iceland zinamenyana leo katika mechi yenye umuhimu mkubwa kwa Argentina.

Katika mechi nyingine iliyofanyika jana timu ya taifa ya Peru ilifungishwa virago baada ya kutandikwa bao moja kwa sifuri na Ufaransa katika kundi C na Australia iligawana pointi na Denmark.