Austria: Afrika ni ufunguo wa utatuzi wa mgogoro wa Wahajiri
Kansela wa Austria amevitaja vikao vya pamoja kati ya Ulaya na Afrika kuwa ni nukta adhimu katika kuupatia ufumbuzi mgogoro wa wahajiri.
Sebastian Kurz ambaye nchi yake hivi karibuni imechukua duru ya uwenyekiti wa Umoja wa Ulaya ameashiria kikao cha Umoja wa Ulaya na Afrika na kueleza kuwa Umoja wa Ulaya siku chache zijazo utaitisha kikao cha pamoja na Afrika; ambapo kinaweza kuwa fursa nzuri kwa ajili ya kushirikiana pande mbili ili kudhibiti mgogoro wa wahajiri.
Kansela wa Austria ameashiria pia kuanza duru ya uwenyekiti wa nchi yake katika Umoja wa Ulaya na kubainisha kuwa katika kipindi cha miezi sita ambapo nchi yake itakuwa mwenyekiti wa kiduru wa Umoja wa Ulaya kutafanyika vikao viwili vya pamoja baina ya Afrika na Ulaya; hatua inayoashiria umuhimu wa nafasi ya Afrika kwa bara Ulaya.
Katika vikao hivyo viwili kutafanyika mashauriano maalumu kati ya Italia, Libya, Uhispania na Morocco. Hii ni katika hali ambayo nchi 14 za Ulaya tayari zimetangaza kuwa ziko tayari kusaini makubaliano ya kuwapokea wahajiri, hata hivyo serikali ya Austria haipo katika orodha hiyo kutokana na kuwa na msimamo mkali kuhusu suala la wahajiri.