Jul 06, 2018 14:25 UTC
  • Waziri Mkuu wa zamani wa Pakistan miaka 10 jela kwa ufisadi

Mahakama ya Kupambana na Ufisadi ya Pakistan imempata na hatia ya ufisadi wa kifedha aliyekuwa Waziri Mkuu wa nchi hiyo pamoja na binti yake na kuwahukumu kifungo cha miaka 10 jela.

Akisoma hukumu hiyo leo Ijumaa katika mahakama hiyo iliyokuwa imefurika katika mji mkuu Islamabad, Jaji Muhammad Bashir amesema mahakama hiyo imempata na hatia Nawaz Sharif, Waziri Mkuu wa zamani wa nchi hiyo pamoja na binti yake Maryam, na imewahukumu kifungo cha miaka kumi jela kila mmoja, mbali na kuwatoza faini ya dola milioni 10.5.

Mwendesha Mashtaka katika keshi hiyo, Sardar Muzaffar Abbasi amewaambia waandishi wa habari kuwa: Hukumu ya leo ya Mahakama ya Kupambana na Ufisadi imeweka wazi kwamba, mali za wawili hao yakiwemo majumba ya kifahari yaliyoko nje ya nchi yalichumwa kwa njia za ufisadi.

Hukumu hiyo inaonekana kuwa pigo kwa chama cha mwanasiasa huyo cha PML-N, na kukikosesha matumaini ya kuibuka mshindi katika uchaguzi mkuu ujao nchini humo.

Nawaz Sharif na wanawe, akiwemo Maryam

Mashtaka hayo ya ufisadi yaliyokuwa yakimkabili Nawaz Sharif, watoto wake wawili wa kiume, binti yake na mkwe wake yanatokana na uchunguzi uliofanywa kupitia nyaraka zilizotolewa na kampuni ya kisheria ya Panama iliyofichua kuwa Sharif anamiliki mali ambazo hajazitangaza nje ya nchi.

Itakumbukwa kuwa, Julai mwaka jana Mahakama ya Juu ya Pakistan ilimtangaza Nawaz Sharif kuwa hana sifa za kuendelea kuwa kiongozi na kumfanya alazimike kujiuzulu kwa tuhuma za ufisadi.

 

Tags