Madaktari Wairani washiriki kumbukumbu ya mauaji ya kimbari Srebrenica
Kundi la madaktari na wasomi wa Iran linashiriki katika kumbukumbu ya 22 ya mauaji ya kimbari yaliyofanywa na Waserbia dhidi ya maelfu ya Waislamu wa Srebrenica huko Bosnia Herzegovina.
Kundi hilo la madaktari wa Iran limejiunga na watu wengine elfu saba kutoka maeneo mbalimbali ya dunia katika matembezi yatakayoendelea kwa muda wa siku tatu kukumbuka mauaji yaliyofanywa dhidi ya Waislamu wa Bosnia. Matembezi hayo ya umbali wa kilomita 110 yameanzia eneo la Nezuk kuelekea Srebrenica.
Ripoti zinasema madaktari wa Iran wanaoshiriki katika matembezi hayo wanatoa huduma ya kutibu na kushughulikia washiriki katika shughuli hiyo ya kukumbuka mauaji makubwa zaidi ya kimbari barani Ulaya baada ya Vita Vya Pili vya Dunia.
Katika shughuli ya mwaka huu ya kukumbuka wahanga wa mauaji ya Srebrenica, mabaki ya maiti ya zaidi ya raia 35 wa eneo hilo yaliyogunduliwa katika maeneo mbalimbali, yatazikwa.
Tarehe 11 Julai mwaka 1995 jeshi la Serbia lililokuwa likiongozwa na Jenerali Ratko Mladić lilivamia mji wa Waislamu wa Srebrenica huko Bosnia Herzegovina na kuua kwa umati Waislamu wasiopungua elfu 8 wa mji huo.
Mauaji hayo yalifanyika mbele ya askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa kutoka Uholanzi ambao hawakuchukua hatua yoyote ya kulinda raia hao.