Russia: Hatutajiondoa katika Shirika Linalopiga Marufuku Silaha za Kemikali
Mwakilishi wa Kudumu wa Russia katika Shirika Linalopiga Marufuku Matumizi ya Silaha za Kemikali amesisitiza kuwa Moscow haina mpango wa kujiondoa katika shirika hilo.
Alexander Shulgin amesema kuwa Moscow haina nia ya kujitoa katika shirika la OPCW licha ya nchi hiyo kupinga suala la shirika hilo kuongezewa mamlaka.
Shulgin ameongeza kuwa, Russia itachukua uamuzi wa kujitoa katika shirika hilo baada ya kufanyika uchunguzi na kuzingatia maslahi ya kitaifa ya nchi hiyo.
Nchi wanachama wa Shirika Linalopiga Marufuku Matumizi ya Silaha za Kemikali (OPCW) tarehe 27 mwezi Juni mwaka huu zilipiga kura zikiunga mkono kuongezewa mamlaka shirika hilo kufuatia pendekezo lililotolewa na Uingereza, ambapo Moscow imepinga hatua hiyo na kueleza kuwa haitaitambua rasmi.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia, Sergei Lavrov pia ameeleza wasiwasi wake kuhusu uamuzi huo na akasema Moscow inafanya jitihada za kubadili uamuzi huo.
Russia na shirika la OPCW zinahitafiana kuhusu madai ya kufanyika shambulio la silaha za kemikali katika mji wa Douma nchini Syria. Uingereza na baadhi ya nchi waitifaki wake wa Magharibi ziliituhumu serikali ya Rais Bashar al Assad wa Syria kuwa imefanya shambulio la kemikali huko Douma; tuhuma ambazo zimekanushwa na serikali ya Moscow.