Tony Schwartz: Rais Donald Trump wa Marekani amepatwa na kichaa
Mwandishi maarufu wa Kimarekani ameelezea hali ya kisaikolojia ya Rais Donald Trump wa nchi hiyo kwamba ni yenye mgogoro na kwamba ni mtu aliyepoteza akili.
Tony Schwartz, ambaye pia ni mwandishi wa kitabu cha 'The Art of the Deal', ameyasema hayo katika mahojiano na kanali ya televisheni ya CNN na kuongeza kuwa, Rais wa Marekani kiujumla amepoteza akili na kwamba hana mawasiliano na ukweli wa mambo.
Kabla ya hapo Schwartz alitangaza kwamba yeye ndiye mwandishi halisi wa kitabu 'The Art of the Deal', ingawa Trump amekisambaza kwa jina lake yeye. Tony Schwartz ameieleza CNN kwamba, siasa za kigeni na ndani za Trump zinaonyesha kwamba usalama wa akili ya mtu huyo umepungua kwa kiasi kikubwa na unakabiliwa na mgogoro.
Ameongeza kwa kusema, hivi sasa Marekani iko katika hali mahututi na kuwa Trump anaendesha nchi kwa mujibu wa hali inayotawala nafsii yake na anayatafsiri mambo kinyume na uhalisia. Amezidi kufafanua kwamba kasi ya kusambaratika akili ya Rais Donald Trump inazidi kuongezeka na jambo hilo ndio sababu inayomfanya rais huyo kutoa maelezo tofauti na yale anayoyatoa kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter.
Kabla ya hapo pia baadhi ya jumuiya za kielimu na asasi za kisaikolojia nchini Marekani zilitahadharisha juu ya kasoro ya kiakili ya Rais Donald Trump na kutokuwa na hadhi ya kuwa rais wa nchi hiyo.