Apr 09, 2016 04:00 UTC
  • Ban Ki-moon atahadharisha kuhusu kuenea hujuma za kundi la Daesh

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametahadharisha kuhusu kuenea harakati za kundi la kigaidi la Daesh kote ulimwenguni.

Akizungumza jana Ijumaa mjini Geneva Uswisi katika kikao cha Kimataifa cha kuzuia kuenea duniani vitendo vya uchupaji mipaka, Ban Ki-moon Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametahadharisha juu ya kuenea harakati za kundi la kigaidi la Daesh kote ulimwenguni na kuzitolea wito nchi zote kushirikiana ili kuendesha vita dhidi ya kundi hilo.

Ban Ki-moon ameongeza kuwa, ushahidi uliopo unaonyesha kuwa radimalai ya kiusalama na kijeshi pekee haiwezi kutoa pigo kwa magaidi.

Didier Burkhalter Waziri wa Mambo ya Nje ya Uswisi pia ambaye alikuwa mwenyekiti wa kikao hicho ameeleza kuwa, suala la kukabiliana na vitendo vya kufurutu ada na misimamo mikali linahitaji kuheshimiwa mamlaka ya kisheria, haki za binadamu na kuheshimiwa sheria za kimataifa katika mapigano ya silaha.

Kikao cha kimataifa cha kuzuia kuenea vitendo vya uchupaji mipaka mjini Gemeva Uswisi kimehudhuriwa na Mawaziri na Manaibu Mawaziri kutoka nchi 30 duniani. Kikao hicho kimefanyika katika hali ambayo kundi la kigaidi la Daesh katika miezi ya hivi karibuni limetenda jinai chungu nzima katika nchi za eneo hili khususan huko Iraq na Syria kwa kuungwa mkono kifedha na kijeshi na Marekani na baadhi ya nchi za Magharibi na Kiarabu.

Tags